Saturday 16 August 2014

inaendelea:UTETEZI WA WA MUUNDO WA SERIKALI MBILI KATIKA MUUNGANO

UTETEZI WA WA MUUNDO WA SERIKALI MBILI KATIKA MUUNGANO
Watanzania wengi hasa vijana na hata ambao ni watu wazima hawajui na hawajapata nafasi ya
kujiuliza kwanini Muungano wetu una serikali mbili na siyo tatu na kwanini serikali hizo ziko jinsi
zilivyo. Kutokana na kutojua hili wengi hufanya haraka na kusema “tuwe na serikali tatu” bila
kujiuliza kama kufanya hivyo kutatua tatizo au la au kutaongeza tu tatizo. Nyerere anawajibu wale
wenye kuhoji haya kwa kuwapa historia kidogo ya mfumo wa Muungano. Kwa kutumia hoja za
kimantiki na kiufundi wa maneno kuonesha kuwa Muungano wa Tanzania ndio nchi pekee katika
Afrika iliyoundwa na Wananchi wenyewe. Tanzania siyo zao la mipaka ya ukoloni au matokeo ya
Mkutano wa Berlin wa 1884-1885 kama zilivyo nchi karibu zote za kiafrika. Nyerere anajenga hoja
kuwa Watanzania wasiwe dhaifu kukumbatia kilichoundwa na mkoloni kuwa ni chao halafu
walichounda wao wenyewe kukibeza na kujaribu kukivunja. Siyo hivyo tu, anashangaa kwanini watu
waone kilichoundwa na mkoloni bila kura ya maoni ya waliotawaliwa au kwa hiari ya wananchi kuwa
ni halali lakini kilichoundwa na wananchi wenyewe kwa makubaliano ya wananchi bila ya kura ya
maoni kuwa ni haramu? Hapa tunaweza kuona tofauti ya ujengaji hoja wa Mwalimu na wale wenye
kutaka kukubaliwa tu bila ya kuwa na hoja zenye nguvu. – M. M.


BUNGENI: 14/8/1993
Kesho yake tarehe 14/8/1993 tulikwenda bungeni.
(i) Nadhani jana yake Waziri Mkuu alikuwa amekwisha kutangaza uamuzi wa Zanzibar kutoka katika
OIC, na wakubali mapendekezo ya Kamati ya Bomani kuhusu utaratibu wa kuchagua Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano. Na kwa upande wa Zanzibar Rais wa Zanzibar alikuwa amekwisha kufanya
hivyo. Bungeni Waziri Mkuu alieleza sababu za kutuomba tuseme na wabunge.
(ii) Rais alieleza historia ya kisa cha OIC na uamuzi wa Zanzibar kujitoa. Akapinga hoja ya Serikali
tatu.
(iii) Mimi nilieleza kwa kirefu sana ile migogoro miwili ya awali. Pia kupinga hoja ya Serikali Tatu.
Katika kufanya hivyo nilieleza historia ya Muungano wa Serikali Mbili, badala ya serikali moja au
shirikisho la serilali tatu.
MFUMO WA SERIKALI MBILI: Kisanduku 1
Nchi mbili zinapoungana na kuwa Nchi moja mifumo ya kawaida ya miundo ya Katiba ni miwili:
Muungano wa Serikali Moja, au Shirikisho la serikali Tatu. Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta
serikali yake na nchi mpya inayolizaliwa itakuwa ni nchi moja yenye Serikali moja. Katika mfumo wa
pili kila nchi itajivua madaraka ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho na itakuwa na serikali
ambayo ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki.
Mambo yatakayoshikwa na serikali ya Shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika nchi zilizungana basi
kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi kuwa nchi moja bali zinaendelea kuwa nchi
mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo fulani fulani.
Nchi za Afrika Mashariki zilikuwa katika hali kama hiyo kabla ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Zilikuwa ni Nchi Tatu zenye ushirikiano mkubwa, lakini hazikuwa Nchi Tatu zilizoungana
kuwa Nchi Moja yenye muundo wa Shirikisho. Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni Nchi Moja
yenye Serikali tatu, Serikali ya Shirikisho, na Serikali mbili za nchi mbili za awali zilizoungana kuzaa
nchi mpya moja.
Tanganyika na Zanzibar zilipoamua kuungana na kuwa Nchi Moja, tungeweza kufuata mmojawapo wa
mifumo hiyo ya kawaida. Lakini tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zanzibar na
ukubwa wa Tanganyika. Zanzibar ilikuwa na watu laki tatu (300,000) na Tanganyika watu milioni kumi
na mbili (12,000,000). Muungano wa Serikali Moja ungefanya ionekane kama Tanganyika imeimeza
Zanzibar. Tulikuwa tunapigania Uhuru na Umoja wa Afrika; hatukutaka tutuhumiwe hata kwa makosa,
kwamba tunaanzisha ubeberu mpya!
Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa Serikali Moja. Shirikisho la Serikali Tatu lingekuwa ni gharama
kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzibar ingeendesha Serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha
Serikali ya Shirikisho; na Tanganyika ingefanya vivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa
Tanganyika ndio hasa ungeendesha SerikaIi ya Shirikisho. Kwa hiyo Tanganyika ingeendesha Serikali
yake ya watu 12, 000, 000 na pia ndiyo ingetoa sehemu kubwa ya kuendesha Serikali ya Shirikisho la
watu 12,300,000.
Ni Watu wanaofikiri kwa ndimi zao wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yoyote kati ya hizo
ingekuwa ndogo. Gharama ya Serikali ya Tanganyika isingekuwa ndogo, (waulizeni Wazanzibari), na
wala ya Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo. Hata bila ya gharama za mambo yasiyo ya
Shirikisho. Na gharama zote hizo kwa kweli zingebebwa na Tanganyika.
Kwa hivyo ilitupasa tujiulize kwa nini tunataka kuibebesha Tanganyika gharama zote hizo; na hasa
kwa nini tunataka Serikali ya Tanganyika? Hivi tuna hofu ya kwamba Tanganyika, bila kuwa na
SerikaIi yake, itaonekana kuwa imemezwa na Zanzibar? Hofu yetu ni kwamba tukiwa na Serikali Moja
Tanganyika itaonekana kuwa imeimeza Zanzibar. Basi na tutafute mfumo ambao utaiondolea
Zanzibar hofu hii ya kumezwa, bila kuibebesha Tanganyika mzigo wa kuendesha Serikalli mbili
zenye uzito unaolingana.
Hivyo ndivyo tulivyofanya, na hiyo ndiyo asili ya muundo wa Muungano wa serikali mbili. Badala ya
kutungua mfumo uliopo kama wapumbavu, tulitazamia hali halisi yetu ilivyokuwa, na tukabuni mfumo
uliotufaa zaidi.
Labda ni vizuri kukumbusha kwamba shabaha ya baadhi yetu ilikuwa ni kuunganisha nchi za Afrika
Mashariki ziwe nchi moja. Na wakati Zanzibar na Tanganyika zinaungana, Kenya, Uganda na
Tanganyika zilikuwa katikati ya mazungumzo ya kutafuta uwezekano, wa kuungana. Kama jambo hilo,
lingetokea, nina hakika kabisa kwamba mfumo wa nchi mpya ambayo ingezaliwa ungelikuwa ni
Shirikisho; au la Shirikisho la Nchi Tatu zenye Serikali Nne au Shirikisho la Nchi Nne zenye Serikali
Tano.
Kwa kweli hata kesho Nchi za Afrika ya Mashariki zikiamua kuungana, na Tanzania ikawa ni mshiriki,
naamini kuwa ni rahisi zaidi kushirikisha Tanzania yenye Serikali Mbili - ya Zanzibar na ya
Tanganyika - kuliko Tanzania yenye Serikali Mbili, ya Tanzania na ya Zanzibar. Wapendao
Utanganyika watakuwa wazalendo zaidi, badala ya kuwa wasaliti, wakiazimia Afrika ya Mashariki
iliyoungana kuwa Nchi Moja. kuliko Tanzania iliyotengana ikawa nchi mbili.
Siku ya pili yake tarehe 15/8/1993, Wabunge wenye hoja yao na wengine zaidi, waliomba tena kuja
'Tunywe chai'. Na baada ya mazungumzo nao ilikuwa ni dhahiri kabisa kwangu kwamba hata kama
hawakuondoa hoja yao (wala mimi sikuwaomba waiondoe), wataitumia kutoa dukuduku zao tu;
hawataitumia kung'ang'ania kudai Serikali ya Tanganyika. Kwa hiyo sikushangaa baadaye niliposikia
kuwa waliiondoa hoja yao ya awali, na badala yake wakaleta hoja ya kutafuta maoni ya wananchi.
Mimi kwa upande wangu nilihisi kuwa hoja mpya hii ilikuwa na shabaha ileile ya "kunawa uso",kama
Zanzibar kusema kuwa wanatoka katika OIC, 1akini utafanywa uchunguzi wa kuona kama Tanzania
inaweza kuingia katika OIC.
Huko nyuma baadhi ya viongozi wa Zanzibar wapinzani wa Muungano wamewahi kudai tufanye
referendum kwa Zanzibar kuhusu Muungano. Tukakataa kwa sababu safi kabisa. Maoni haya ya

Wabunge wa Bara ambao mimi naamini kabisa si wapinzani wa Muungano, nayo yangeweza
kukataliwa na Chama na Serikali kwa sababu zile zile na mambo yakesha.II
                                            
                                                        SURA YA TANO
                                             SERIKALI ILIPOSALIMU AMRI
Nyerere aliamua kuvunja mzizi wa fitina kwa kuchambua jambo moja muhimu sana ambalo hata
baadaye lingetusaidia kama tungeona umuhimu wake kuanzia wakati huo. Kwamba, uongozi mara
zote ni kuongoza siyo kufuata. Nyerere alisikitishwa sana na kitendo cha viongozi wetu kushindwa
kuonesha uongozi na badala yake kulazimika kufuata. Ulikuwa ni udhaifu ambao kama ungekubaliwa
basi ungesababisha kusambaratika kwa Tanzania kama tuijuavyo. Analolisema hapa lina ukweli hata
leo hii tunapoendelea kuhangaika na uongozi wetu kwani mara kadhaa tumeona jinsi ambavyo
viongozi wetu wanafuata matukio na hali badala ya kuonesha uongozi kukubali matatizo kabla
hatujafika mbali. Kile ambacho Nyerere anakiita “kusarenda” kimejirudia tena na tena katika taifa
letu tangu wakati wa kijitabu hiki kutolewa. Tumeona haya kwenye masuala ya EPA, Meremeta,
Richmond/Dowans n.k Nyerere anasema “kuongoza ni kuonesha njia”, hii ni kauli yenye ukweli
mkubwa sana kwani endapo mtu anayeitwa kiongozi anashindwa kuonesha njia basi kiongozi huyo
yampasa aachie ngazi ili waje watu wanaoweza kuonesha njia siyo kufuata. – M.M
Baadaye, nadhani siku iIiyofuatia niliitisha kikao cha Watangazaji wa Habari nikapinga kwa kirefu
hoja ya Utanganyika. Wakati naondoka Dar es Salaam ili kurudi Butiama nilitumaini kabisa kwamba
Serikali ingeendeleza Bungeni na kama hapana budi nchini kazi tuliyoanza pamoja ya kupinga hoja ya
Tanganyika. Sikuwa na sababu yoyote ya kuhofia kuwa siku chache tu baadaye Serikali itageuza
msimamo wake na kufanya "abautani".
Sijui lililotokea, maana kila nilipouliza sikupata maelezo. Kama nilivyokwisha kusema hapo nyuma
baadaye wabunge wahusika waliiondoa hoja yao ya awali ya kutaka Bunge lipitishe azimio la kudai
Serikali Tatu, wakaleta hoja mpya ya kutaka Serikali ifanye referendamu ya kutafuta maoni ya
wananchi kuhusu suala hili. Nasema, Serikali ingeweza kuikataa hoja hii kwa maelezo safi kabisa na
mambo yakesha.
Au kama wangeona kuwa si siasa nzuri kuipinga hoja hii nayo wangeweza kuikubali; na mimi nina
hakika wananchi wangeikataa na mambo yakesha. Lakini Serikali ya Muungano bila maelezo ilikataa
hoja mpya ya wabunge ya kutaka maoni ya wananchi na yenyewe ndiyo ikafufua hoja ya Utanganyika,
na kupendekeza kwamba badala ya hoja ya Serikali Tatu kujadiliwa Bungeni na kupigiwa kura Bunge
zima pamoja na Serikali yenyewe likubali hoja hiyo, bila mjadala!
Kumbe jambo ambalo viongozi wetu walikuwa wanahofu kabisa kabisa ni mjadala, maana huo

ungewalazimisha kujitambulisha kama si katika mjadala wenyewe basi wakati wa kupiga kura hasa
ikiwa ni kura ya kuita mbunge mmoja mmoja kwa jina pamoja na mawaziri wetu! Badala ya kupita
katika adha hiyo wakaona afadhali wakubali Serikali Tatu bila ya mjadala. Basi SerikaIi yetu ikanywea
ghafIa kama mpira uliotoboka au puto lililopasuka. Nadhani hata wabunge wenye hoja ya awali
walishangaa!
Kuongoza ni kuonesha njia. Viongozi wetu walikuwa wametumwa na chama chao waende bungeni,
Bunge la wanachama watupu wa CCM wakawaoneshe njia. Wakawaambie wabunge wahusika
kwamba hoja yao ya kutaka Serikali Tatu ni kinyume cha sera ya chama chao na ina hatari ya kuigawa
na kuiangamiza Nchi yetu.
Waliagizwa wazi wazi wakaipinge hoja hiyo. Wakapata mtihani mdogo sana bungeni.
Wakasarenda. Wakatupa silaha chini; wakasalimu amri. Viongozi hawa hawawezi kusimama mbele ya
Kamati Kuu au mbeIe ya Halmashauri Kuu ya Taifa kusema kwa fahari kama wao ni hodari: Kazi
mliyotutuma tumeikamilisha! Wala hawataki kukubali matokeo ya kusarenda kwao.
Kwa sababu uamuzi wa kutaka Serikali ya Tanganyika ‘ndani ya muungano’ ulifanywa na viongozi
wetu kwa hila na kupitishwa bungeni bila mjadala sisi wengine hatukujua lililotokea. Baadaye
tulifahamishwa kuwa huo ndiyo ulikuwa uamuzi wa ‘bunge zima” kutokana na kauli ya Pius Msekwa
aliyekuwa msimamizi wa kikao cha Bunge kilichofikia uamuzi huo. Nadhani viongozi wetu walitaka
kuendelea kuficha na kuuvuga vuga, lakini yeye akatoboa. Nasikia baadaye aliitwa akakemewa. Sijui
kwa nini.

KUTAFUTA UFAFANUZI WA KUSALIMU AMRI KWA SERIKALI
DODOMA II 14/10/1993

Nilipokwisha kuhakikishiwa kuwa sasa sera ya Serikali Tatu ndiyo sera rasmi ya Bunge la Muungano
na Serikali ya Muungano nilijaribu kupata maelezo kutoka kwa viongozi wetu lakini sikufanikiwa.
Waziri mkuu nilipomuuliza kama kweli wamebadili sera alicheka tu! Nilikuwa na safari ya
kutembelea nchi za Asia kwa ajili ya shughuli zinazotokana na uenyekiti wangu wa Tume Nchi za kusini.
Niliporudi kutoka safari nilijaribu tena kuonana na viongozi wetu ili nipate maelezo lakini sikufanikiwa
kumpata kiongozi yeyote mhusika. Nilipopata habari kwamba halmashauri Kuu ya Taifa itakutana
Dodoma nilihisi kuwa bila shaka viongozi wetu wataeleza kwa nini wameacha msimamo wa Chama na
maagizo ya Kamati Kuu ya kupinga hoja ya Utanganyika, wakaamua kukubali hoja hiyo. Basi
nikaomba angalau nipatiwe nafasi nihudhurie kikao hicho cha Halmashauri kuu ya Taifa ili nami
nisikie maelezo watakayotoa. Baada ya maajabu ambayo haina maana kuyaeleza nilikubaliwa nikaenda
Dodoma.
KIKAO CHA FARAGHA
Safari hii tulikuwa na vikao viwili. Kwanza kikao cha faragha wakiwapo viongozi wakuu wote wa
Chama na Serikali, na wengine wa nyongeza. Kilikuwa kikao kirefu na kigumu. Sina kawaida ya
kulizwa na mambo ya siasa lakini katika kikao hiki nilishindwa kujizuia kulia. Sikupata maelezo
ya maana ya kuwafanya watu wafanye walivyofanya. Nilipouliza kwa nini hawakupinga hoja ya
Serikali tatu kama tulivyokuwa tumekubaliana majibu ya viongozi wetu wakuu yalikuwa ni ya ajabu
kabisa. Ati wabunge wenye hoja baada ya kuonana na mimi Msasani walikwenda Bungeni wakiwa
wakali kama mbogo! Tena walikuwa wakiwatukana wenzao (yaani wabunge wa Zanzibar) kwa
kuwataja majina.
Hizi ni sababu za ajabu sana za kuwafanya viongozi watu wazima watelekeze msimamo mzima wa
Chama chao na makubaliano ya watu makini kuutetea msimamo huo na waamue kuikumbatia hoja ya
mbogo wakali! Huu ni uongozi wa ajabu kabisa!
Nilipowabana zaidi niliahidiwa kuwa maelezo mazuri yatatolewa kesho yake na waziri wa Sheria na
mambo ya katiba katika kikao cha Halmashauri Kuu ya taifa.
 
KIKAO CHA HALMASHAURI KUU:
Hakika siku ya pili yake waligawiwa ‘TAARIFA YA SERIKALI JUU YA AZIMIO LA BUNGE
KUHUSU HAJA YA KUUNDA SERIKALI YA TANGANYIKA NDANI YA MUUNDO WA
MUUNGANO’. 

Taarifa yenyewe ni ndefu ina maelezo mengine ya mapambo tu, au ya kiini macho.
Lakini vipengele vinavyohusika na suala lenyewe vilikuwa vichache na nimevinukuu kwa ukamilifu
(tazama kisanduku 2)
“9: Tarehe 30 Julai, 1993 wakati wa mkutano wa bunge la bajeti ukiendelea, zaidi ya wabunge 50 kwa
pamoja walitoa taarifa ya kusudio la kuwasilisha hoja Bungeni ambayo inadai miongoni mwa mambo
mengine;
Kwa kuwa kuendelea mfumo huu wa Muungano usiowaridhisha wananchi wengi wa upande mmoja ni
kuhatarisha kuendelea na kudumu kwa Muungano na pia kuathiri uelewano kati ya watu pande zote
mbili; na
Kwa kuwa uwezekano wa kuunda serikali moja ya Jamhuri ya Muungano kwa nchi nzima kwa mambo
yote haujajionesha;
Hivyo basi wabunge hawa wanaliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano katika mkutano wake wa kumi
na mbili unaofanyika Dar Es salaam liazimie kwamba;
Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilete Muswada Bungeni kabla ya Februari 1994, kurekebisha katiba
ya Jamhuri ya Muungano ili kuwezesha uundaji wa “Serikali ya Tanganyika” ndani ya Muungano.
Tarehe 12 Agosti, 1993 hotuba ya kuwasilisha Makadirio ya Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba
ilisomwa Bungeni. Katika hotuba hiyo Serikali ilieleza kusudio la kuandaa waraka wa Serikali (White
Paper) kutafuta maoni ya wananchi kuhusu muundo wa Muungano. Tarehe 20 Agosti, 1993 wabunge
wahusika waliwasilisha taarifa nyingine inayobadilisha ile hoja ya awali iliyosambazwa kwa wabunge
wote. Hoja mpya ilikuwa inalitaka Bunge zima liazimie kwamba:
Serikali ya Jamhuri ya Muungano iandae kura ya maoni ambayo itafanyika kabla ya 31 Desemba,
1994 ili kupata maoni ya wananchi wa Tanzania juu ya kuundwa kwa “Serikali ya Tanganyika” ndani
ya Muundo wa Muungano utakaozingatia mabadiliko hayo. Kutokana na taarifa hizi, Baraza la
Mawaziri lilifanya kikao cha dharura ili kutafakari taarifa hizi na athari zake kama zingewasilishwa
Bungeni na kupigiwa kura.

Kwanza kabisa, inaonekana kwamba hoja ya awali ingekuwa vigumu kutekelezeka kutokana na muda
mfupi uliowekwa kufikia Februari 1994, na pia haikutoa fursa kupata maelekezo ya Chama wala
serikali zetu mbili kushauriana. Kwa kutambua kwamba Bunge linafanya maamuzi yake kwa njia ya
kura baada ya mijadala ya wazi, Serikali iliona kwamba hoja yote kati ya hizi ingewasilishwa
Bungeni, ingeweza kuligawa Bunge, kukigawa chama chetu na kuwagawa wananchi katika suala zito
kama hili la Muundo wa muungano.
Kuhusu suala la kura ya maoni serikali iliona kwamba utekelezaji wake ni sawa na kufanya uchaguzi
mkuu, jambo ambalo ni la gharama kubwa. Aidha, kwa kuzingatia kwamba kura ya maoni kupigiwa
suala linalohitaji jibu la ‘NDIYO’ au ‘HAPANA’ , ni vigumu kupata swali lililo wazi kwa wananchi
ambao hawana uzoefu wa utaratibu huo wa kura ya maoni.
Pamoja na hayo, kwa kuzingatia kwamba uamuzi wa kura ya maoni ni lazima ukubalike katika sehemu
zote mbili za Muungano, itakuwa vigumu kupata uwiano wa kura utakaokubalika pande zote mbili
kuwa ndio kiwango cha uamuzi.
10. Pamoja na juhudi za Serikali zote mbili kupitia Kamati ya Pamoja, Serikali zetu pia zilifikia
makubaliano na kufanya maamuzi kuhusu baadhi ya matatizo mazito yaliyokuwapo katika Muungano
wetu. Maamuzi hayo ni:
(a) Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kukubali Zanzibar kujitoa katika uanachama wa 'OIC';
(b) Utaratibu wa kumpata Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano uwe ni kwa njia ya kupigiwa
kura kwa pamoja na mgombea urais (running mate).
11. Kwa msingi huu na kwa kuzingatia maamuzi ya awali ya Serikali ya kutaka kupata maelekezo ya
chama na maoni ya wananchi kuhusu muundo utakaotatua matatizo ya Muungano, Serikali iliona kuna
umuhimu wa kushauriana na wabunge waliohusika ili kupata muafaka wa maudhui ya hoja yenyewe.
Muafaka huo ulifikiwa katika Kikao cha Kamati ya Wabunge wakikaa kama Kamati ya Chama tarehe
12/8/93. Kutokana na muafaka huo hoja ya wabunge ilirekebishwa na azimio la Bunge kupitishwa kwa
kauli moja kwamba:
"Serikali iandae na kusimamia utaratibu utakaoshirikisha wananchi na taasisi mbali mbali ili
kufikisha Bungeni kabla ya Aprili, 1995, mapendekezo ya muundo muafaka wa Muungano ambao
utazingatia haja ya kuwapo Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano pamoja na mambo mengine.
12. Azimio hili linaagiza mambo mawili yaliyo wazi:
(a) kupatikana kwa muundo muafaka wa Muungano ambao unazingatia haja ya kuwapo Serikali ya
Tanganyika.
(b) Kuwapo na utaratibu wa kushirikisha wananchi na taasisi mbalimbali utakaosimamiwa na Serikali
kabla ya mapendekezo ya mwisho kufikishwa Bungeni.
13. Kwa kuwa suala la muundo wa nchi ni zito na ni la kikatiba, ushirikishwaji wa wananchi ni jambo
lisiloweza kuepukwa. Aidha kwa uzoefu wetu na hali halisi ya nchi yetu, ni lazima utaratibu wo wote
utakaokubalika, uwezeshe Serikali yaJamhuri ya Muungano kushauriana na Chama na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar.
 
Hatua za Serikali baada ya azimio na mapendekezo
14. Kutokana na Azimio la Bunge, Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeona kwamba suala la muundo
wa Muungano sasa linahitaji kufanyiwa kazi na kupatiwa uamuzi haraka zaidi na hivyo ni muhimu
kuwasilishwa kwenye Chama mapema kwa maelekezo, bila kusubiri mapendekezo ya Kamati ya
pamoja i1i kuondoa hisia kwamba Serikali inajaribu kulikwepa suala hili.
15. Katika hali hii, Serikali inapendekeza kwamba Halmashauri Kuu ya Chama iafiki pendekezo la
Serikali la kuandaa Waraka wa Serikali wa kutafuta maoni ya wananchi (White Paper) kuhusu
muundo muafaka wa Muungano kwa kuzingatia mambo yafuatayo:
(a) Dhana ya kuwa na Serikali tatu ndani ya Muungano, yaani Serikali ya Muungano, Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Tanganyika ikubalike. Muungano wa aina hii kwa Sheria za Katiba
na za Kimataifa ni wa Shirikisho (Federation).
(b) Kwamba muundo uwe ni Muungano wenye Serikali tatu, yaani Serikali ya Muungano, Serikali ya
Tanganyika na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. lkumbukwe kwamba neno Muungano linavyofahamika
kwenye Sheria za Katiba na za Kimataifa linamaanisha kwamba majukumu yale ya msingi ya dola
yanahamishiwa kwenye Serikali ya Muungano."
Haya ni maelezo ya ajabu sana kutoka kwa watu wazima kwenda kwa watu wazima wengine.
"Kwanza kabisa", Serikali yetu inaiambia Halmashauri Kuu ya Taifa, "inaonekana kuwa hoja ya awali
ingekuwa vigumu kuitekeleza kutokana na muda uliowekwa kufikia Februari, 1994, na pia haikutoa
fursa ya kupata maelekezo ya Chama wala Serikali zetu mbili kushauriana.
Aidha, "Kwa kutambua kwamba Bunge linafanya maamuzi yake kwa njia ya kura baada ya mijadala ya
wazi wazi, Serikali iliona kwamba hoja yo yote kati ya hizi ingewasilishwa bungeni ingeweza kuligawa
Bunge, kukigawa chama chetu na kuwagawa wananchi katika suala zito kama hili la Muundo wa
Muungano."
Kwanza, hii "hoja ya awali" ambayo waheshimiwa hawa wanasema hawakuwa na muda wa kutosha
kuitekeleza ni ile ya kutaka Serikali Tatu ambayo kwanza, ni kinyume na sera ya Chama; pili,
walikuwa wameagizwa na Kamati Kuu ya CCM siku chache zilizopita wakaipinge Bungeni; Tatu,
tarehe 12 Agosti, 1993, Serikali yenyewe ilikuwa imeliambia Bunge kwamba ilikuwa inaandaa waraka
wa kutafuta maoni ya wananchi kuhusu suala hili; na nne, (na pengine kutokana na kauli hii ya
Serikali) tarehe 20 Agosti, 1993, wabunge wahusika walikuwa wamekwisha kuondoa hoja yao ya awali
nao wakaleta hoja mpya: ya kuitaka Serikali ifanye referendamu ya kutafuta maoni ya wananchi.
Labda waheshimiwa wabunge nao waliona kuwa hoja hii ya kudai Serikali tatu "ikiwasilishwa
Bungeni, ingeweza kuligawa Bunge, kukigawa Chama chetu; na kuwagawa wananchi katika suala zito
kama hili la Muundo wa Muungano." Mimi siamini hivyo; naamini kuwa kama ingewasilishwa
bungeni ili ijadiliwe, ingejadiliwa ikakataliwa na mambo yangeisha Maamuzi yoyote ya
kidemokrasia hayana budi yatokane na mjadala. Bila ya mjadala, maamuzi, hata yaliyo muhimu
kabisa yatafanywa kwa nguvu ya hila. Lakini kwa vyo vyote vile, hoja hii Wabunge wahusika
walikwisha kuiondoa.
Kama viongozi wetu waliamini kuwa kujadiliwa kwake kutaleta mgawanyiko huo waliouhofu, kwa
nini basi wakati CCM ilipotaka kubadili sera yake haikutafuta kwanza maoni ya wananchi?
Halmashauri Kuu ya Taifa iliketi Unguja ikabadili Azimio la Arusha bila kwanza kutafuta maoni
ya wananchi. Na walikuwa na haki kufanya hivyo, maana sera ni yao. Ubaya wao ni kwamba jambo
lenyewe walilifanya kwa hila na 'janja janja", na mpaka sasa wanaendelea kudanganya wananchi

kwamba sera ya CCM bado ni Ujamaa na Kujitegemea.
Ndivyo viongozi wetu waheshimiwa wanavyojaribu kufanya hata katika suala hili la Muungano.
Wanataka kuvunja Tanzania maana "wamechoka na Wazanzibari"; lakini hawataki kusema hivyo wazi
wazi. Wanachosema ni kwamba wanataka Serikali ya Tanganyika "ndani ya Muungano", ingawa
wanafahamu, maana si watu wapumbavu, kwamba ukifufua Tanganyika utaua Tanzania.