Tuesday 19 August 2014

MAREKAN NA UBAGUZI WA RANGI:Mapigano yazuka upya Missouri

Mapigano yazuka upya Missouri

 19 Agosti, 2014 

Rais Obama amehimiza kuwe na utulivu
Maafisa wa polisi huko Marekani walirusha mabomu ya machozi ili kutawanya halaiki ya watu waliokuwa wakiandamana , kwa usiku mwingine, katika mji wa Ferguson, jimbo la Missouri kupinga mauaji ya kijana mweusi.
Maandamano yalitibuka saa chache baada ya hotuba ya Rais Obama akisihi raia kuwa watulivu.
Chanzo cha maandamano hayo ni kuuawa kwa kijana mmoja mweusi, aliyepigwa risasi na maafisa wa polisi tarehe 9, mwezi huu.
Michael Brown, ambaye hakuwa na silaha yoyote, alipigwa risasi mara sita na polisi waliomshuku kuwa alikuwa ametekeleza wizi wa kimabavu katika duka moja mjini Ferguson.
Mwanasheria mkuu wa Marekani anatarajiwa kuzuru mji wa Ferguson atakapokutana na maafisa wanaopeleleza mauaji hayo.
Gavana wa Missouri Jay Nixon aliidhinisha kutumika kwa kitengo maalum cha polisi wa kuzima ghasia waliotumwa eneo hilo hapo jana ili kusaidia juhudi za polisi kurejesha amani, huku amri ya kutoruhusiwa kutoka nje iliyotangaza mwishoni mwa wiki iliyopita ikiondolewa.
Kuuwawa kwa Brown na askari mzungu kulizusha wasiwasi kati ya watu wa rangi tofauti katika eneo hilo, Ferguson, lililo na jamii yenye wakazi wengi weusi.
Afisa wa polisi Darren Wilson alimpiga risasi Michael Brown juma lililopita baada ya kumsimamisha kwa kutembea barabarani, kulingana na ripoti zilizotolewa.
Afisa mkuu wa polisi Ron Johnson, anayeendesha operesheni hiyo ya Ferguson, alisema maafisa wa polisi walilazimika kuingia mjini humo siku ya Jumanne, baada ya waandamanaji kuwashambulia kwa bunduki na kuwarushia mabomu ya petrol na machupa huku watu wawili wakipata majeraha ya risasi.
Alisihi waandamanaji kufanya maandamano yao nyakati za mchana ili kuzuia “baadhi ya wahalifu” kuanzisha vurugu kimakusudi.
"Yeyote ambaye amewahi kushiriki katika maandamano kama haya anafahamu kuwa kuna hatari nyakati za usiku: maandamano ya usiku huruhusu wahalifu wachache kujificha miongoni mwa halaiki ya watu na kujaribu kuleta vurugu,” Jonson alisema.
Maafisa wa polisi wakiwakamata waandamanaji Ferguson
Maafisa wa usalama pia waliamuru wanahabari kuondoka baada ya waandamanaji walikataa kutoa vizuizi barabarani.
Ushahidi wa video unaonyesha maafisa wa polisi wakiwakamata waandamanaji kadhaa, huku msururu wa maafisa wa polisi waliojihami wakiingia kukabiliana na umati wa watu waliojawa na hasira.

Matukio Ferguson

  • 9 Agosti: Michael Brown apigwa risasi na afisa Darren Wilson.
  • 10 Agosti: Machafuko yaanza kutokota baada ya watu kukesha kwa ajili ya mauaji yake .
  • 11 Agosti: FBI yaanzisha uchunguzi wa mauaji ya kijana huyo.
  • 12Agosti:Wasiwasi yaenena, huku maafisa wa polisi wakitumia mabomu ya machozi na risasi za raba kutawanya.
  • 15 Agosti: Maafisa wa polisi watoa kanda ya video inayosemekana kuonyesha Brown akiibakatika duka Fulani.
  • Video hiyo ilikera waandamanaji hata zaidi na kusababisha mapigano mapya kati ya raia na polisi.
  • 16 Agosti: Missouri yatangaza hali ya tahadhari na kutoa amri ya kutotoka nje katika mji wa Ferguson.
  • 17 Agosti: Gavana Jay Nixon atuma kitengo maalum cha polisi wa kukabiliana na ghasia.
  • 18 Agosti: Uchunguzi ulioagizwa na familia ya Brown wadhibitisha alipigwa risasi sita, mbili za kichwani.
Mpigapicha anayefanyia shirika la Getty, ni mmojawapo ya waliotiwa nguvuni, hata hivyo aliachiliwa huru baadaye.
Katika taarifa ya hapo awali, mwanasheria mkuu wa Marekani Eric Holder alisema “atazuru eneo hilo binafsi” hapo kesho ili kupatana na wapelelezi kutoka kwa ofisi ya uchunguzi FBI na waendesha mashtaka.
"Watu wanataka kufahamishwa yaliyojiri na kupelekea Michael Brown kuuawa, lakini nasihi raia wawe watulivu huku tukiendeleza upelelezi,” bwana Holder alisema.
Pia alisisitiza kuwa uchunguzi huo “ulikuwa hatua ya muhimu ili kurejesha imani kati ya watekelezaji wa sheria na jamii, sio tu katika eneo la Ferguson, bali hata katika maeneo mengine.”
wakati huohuo Rais Obama alielezea kuwa anaelewa “hisia za mapenzi na hasira” zinazozushwa kufuatia mauaji ya kijana huyo.
Matukio kulingana na nyakati
Lakini alisema,vitendo vya hasira, “kuiba au kujihami kwa bunduki, au hata kushambulia maafisa wa polisi, ni vichochezi vya ghasia zaidi.”
Rais Obama alisema alitambua kuwa katika jamii nyingi nchini Marekani “kulikuwepo na “ghuba la kutoaminiana” kati ya wakazi na watekelezaji wa sharia.
"Katika jamii nyingi, vijana wengi wa rangi huwachwa nyuma na hutazamwa kuwa watu wa kuogofya,” Rais Obama alisema.
Hapo awali, familia ya Michael Brown ilimtumia daktari mmoja, kufanyia uchunguzi wa mwili wa Micheal.
Daktari huyo, Michael Baden, alisema kuwa aliamini kuwa Brown alipigwa risasi sita.
“Brown angeweza kuishi hata baada ya majeraha hayo yote ya risasi, lakini risasi aliyopigwa kichwani ilisababisha kifo chake,” alisema.
Rais Obama amehimiza kuwe na utulivu
Daktari Baden alisema hakukuwepo na dalili zozote za mapambano, kwani huenda alipata chembe za kutu usoni alipoanguka kwenye veranda baada ya kupigwa risasi.
Aidha Baden aliamini kuwa afisa Wilson hakumpiga risasi Brown akiwa hatua za karibu naye, kwani hakukuwepo na masalio ya baruti kwa mwili wa Brown, ishara kuwa afisa huyo alikuwa zaidi ya futi mbili mbali na Brown.
Mashahidi wamesema kuwa Brown alipigwa risasi akiwa ameinua mikono yake juu akiwa amesalimu kwa amri, huku maafisa wa polisi na wanaomtakia mema Wilson wakisema kuwa Wilson alifyatua risasi wakipigana na Brown.
Afisa huyo aliyempiga bwana Brown risasi, Darren Wilson, aliachishwa kazi bila malipo kufuatia mauaji hayo, huku familia ya bwana Brown ikitoa wito akamatwe na kufunguliwa mashata .
Uchunguzi mwingine utafanyiwa mwili wa Brown na idara ya haki ya Marekani, kuongezea kwa makadirio ya Baden na maafisa wa County ya St. Louis.