Wapinga ndoa kati ya Muarabu na Myahudi
18 Agosti, 2014
Wayahudi wanne wenye msimamo
mkali wamekamatwa nchini Israeli baada ya kuzua rabsha katika sherehe ya
kuadhimisha harusi ya mwanamke myahudi aliyebadili dini na kuwa
Muislamu na kisha kuolewa na mwanamume Mwarabu raiya wa Israeli.
Mamia ya watu waliandamana nje ya ukumbi
uliotumika kwa sherehe hiyo katika mji wa Rishon LeZion Jumapili
wakipinga ndoa hiyo licha ya kuwepo kwa maafisa wa Usalama.Bwana harusi , Mahmoud Mansour, alikuwa amechukua hati ya mahakama ya kupinga kufanyika kwa maandamano ya kupinga nikaha yake lakini maafisa wa usalama wakashindwa kuzima maandamano hayo.
Muungano wa wayahudi wenye msimamo mkali Jewish Lehava walipewa ruhusa ya kuandamana kupinga ndoa hiyo ilimradi tu wasikaribie chini ya mita 200 karibu na ukumbi wa sherehe hiyo.
Kundi hilo linapinga ndoa kati ya Wayahudi na Waarabu.
Waandamanaji wanne walikamatwa na polisi kwa kukiuka masharti yao kulingana na mtandao wa habari wa kiyahudi.
Sadfa ni kuwa kundi lingine linalounga mkono ndoa kati ya Waarabu na Wayahudi lilifanya maandamano kuunga mkono ndoa hiyo na hivyo kuwalazimu maafisa wa usalama kufanya kazi ya ziada kuzuia makabiliano baina ya makundi hayo hasimu.
Bi Malka, 23, alikuwa amesilimu kabla ya sherehe hiyo kuambatana na desturi za kiislamu.
"Kwa kweli tunaishi pamoja kwa amani na sielewi kwanini ndoa hii inawahusu watu." alisema bwana Mansour, 26.
Rais Rivlin alifananisha maandamano hayo dhidi ya ndo hiyo na ''panya anayengata msingi wa unaoliunganisha taifa hilo la Israeli''.