Thursday 18 September 2014

JIPU HILO::RAIS KUTOKUWA NA ‘MENO’ KWENYE BUNGE LA KATIBA ALAUMIWE NANI?

KWANZA kama ilivyo ada nimshukuru Mungu kwa kuniweka hai nikiwa na afya njema.
Wiki iliyopita nilieleza jinsi muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulivyozitesa serikali za muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar. Nikasema kamati na tume nyingi ziliundwa na fedha za walipa kodi, nyingi zikatumika lakini mgogoro upo palepale.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete
Kuna walioshauri kuwa rais alivunje bunge lakini Mwanasheri Mkuu wa Serikali, Frederick Werema akasema, hawezi kulivunja kwa sababu sheria haimruhusu, kwa maneno mengine hana meno ya kumaliza tatizo.
Lakini sasa imedhihirika kuwa hatima ya Bunge Maalum la Katiba imebaki mikononi mwa Rais Jakaya Kikwete, yuleyule aliyetajwa kuwa hana mamlaka ya kulivunja baada ya kuandikiwa barua na uongozi wa bunge hilo akitakiwa atoe ufafanuzi wa kisheria kuhusu tarehe ya mwisho ya kumaliza vikao vyake lakini pia alikutana na wapinzani wa serikali yake.
Ameandikiwa barua kutokana na muda uliopangwa kwenye ratiba ya bunge hilo kuzua utata wa kisheria na kuwapo uwezekano wa mwingiliano na Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi (BLW), Zanzibar.
Ratiba ya Bunge Maalum la Katiba inaonyesha kuwa limepanga kuhitimisha vikao vyake mwishoni mwa Oktoba, tofauti na tarehe iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete Julai 28, mwaka huu ambayo ilitangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) namba 254 la Agosti Mosi.
Tangazo la rais linaonyesha kuwa awamu ya pili ya Bunge Maalum ingeanza Agosti 5, 2014 na kumalizika Oktoba 4, lakini ratiba ya Bunge hilo inaonyesha kuwa litamalizika Oktoba 31, siku ambayo Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samwel Sitta anatakiwa akabidhi kwa rais Katiba inayopendekezwa.
Hadi tunapoandika makala haya serikali bado haijatoa tangazo lingine kwenye gazeti la serikali kuongeza muda hadi mwishoni mwa Oktoba kama alivyosema Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Sitta wakati akitoa ufafanuzi wa siku 60 zilizotengwa kwa ajili ya Bunge hilo, Agosti 5, mwaka huu.
Sitta alisema kwa kadiri ya tafsiri, siku za kazi ni Jumatatu hadi Ijumaa ambazo wajumbe wanapaswa kufanya kazi na kwamba Jumamosi na Jumapili siyo sehemu ya siku 60 zilizoongezwa na rais.
Kuna mchanganyiko mkubwa kwani Katibu wa Bunge Maalum, Yahya Khamis Hamad alisema  hawajapata maelekezo ya ziada kutoka serikalini ambako waliiandika barua ya kuomba ufafanuzi wa kisheria kuhusu suala hilo.
Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alikiri ofisi yake kupokea barua kutoka Bunge Maalum ikiomba ufafanuzi ambao ungeliwezesha kuongeza siku kwa lengo la kukamilisha kazi ya kujadili na kuandika katiba inayopendekezwa na kwamba maombi yao bado yanafanyiwa kazi.
Utata wa kisheria
Licha ya ahadi iliyotolewa na Sitta ni dhahiri kwamba suala hilo lina utata wa kisheria kutokana na kauli iliyowahi kutolewa na Mwanasheria wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema wakati akitoa ufafanuzi wa maana ya siku 70 ambazo bunge lilikaa mara ya kwanza.
Baada ya kusoma hati ya rais ya kuitishwa kwa bunge hilo, Februari mwaka huu, Jaji Werema alisema siku 70 zilizotolewa kwa mujibu wa tangazo la serikali ni za kikalenda na siyo siku za kazi kwa sababu wajumbe wa Bunge Maalum siyo watumishi wa kuajiriwa.
Kauli ya Jaji Werema haijawahi kutenguliwa na Mahakama au yeye mwenyewe na kwa msingi huo, kwenda kinyume chake ni kuvunja Sheria ya Kazi na Majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268 ya 2005.
Mgogoro mwingine unaojitokeza ni ratiba za vikao vya Bunge la Muungano ambalo limepangwa kuanza Novemba 4, 2014 na Baraza la Wawakilishi ambalo limepangwa kukutana kuanzia Oktoba 22, mwaka huu.
Kwa kawaida, vikao vya Bunge hutanguliwa na wiki mbili za vikao vya kamati za kudumu na ikiwa ratiba itabaki kama ilivyo, basi vitaingiliana na vikao vya Bunge Maalum ambalo ratiba yake imepangwa kuendelea hadi Oktoba 31, mwaka huu.
Hakuna ambaye atabisha nikisema kuwa  kwa jinsi ratiba ya Bunge Maalum la Katiba ilivyopangwa lazima itaingilia shughuli za Bunge la Muungano na lile la Baraza la wawakilishi hivyo uamuzi unapaswa ufanywe ili kuepusha mgongano huo.
Njia pekee ni kumuomba Rais Kikwete asogeze mbele vikao vya mabunge mengine ili Bunge Maalum la Katiba lipate nafasi ya kuendelea na kikao japokuwa wapo walioona kuwa hana uwezo wa kulisitisha au kusogeza mbela vikao vyake.
Hakika masuala haya ni mazito na yanatakiwa kutafutiwa ufumbuzi haraka. Lakini wengi tunajiuliza, waliokuwa wakipanga vikao vya Bunge Maalum la Katiba walikuwa hawayajui hayo? Au ni kutaka kumchosha rais bure na kumsababishia atupiwe lawama?
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

No comments:

Post a Comment