Monday 15 September 2014

WAZO LA YANGA::Okwi wa Kazi Gani Jaja Mpango Mzima,

TRAIKA mpya Mbrazili aliyekuwa akikejeliwa na mashabiki wa Yanga, Genilson Santos ‘Jaja’ jana Jumapili amepiga bao mbili kati ya tatu zilizoipa ushindi timu yake dhidi ya Azam na kushangilia kwa ishara ambazo mashabiki walizitafsiri kwamba alikuwa akiwauliza; “Okwi wa kazi gani Yanga?”

Awali kabla ya dirisha la usajili halijafungwa kulikuwepo na mzozo baina ya Kocha Marcio Maximo na uongozi wa timu uliotaka straika aliyejiunga na Simba, Emmanuel Okwi abaki Yanga na Jaja akatwe kwa madai kwamba ni mzito na hayuko fiti kama Okwi aliyelipwa fedha nyingi.

Lakini Maximo akashikilia msimamo wake kwamba Jaja ndiye chaguo lake na Okwi hatacheza Yanga kutokana na utovu wa nidhamu na kususa mara kwa mara.Licha ya kuwathibitishia Yanga kwamba yeye ni mashine na amesajiliwa kwa ajili ya kufunga tu, Jaja jana aliwaziba midomo mashabiki wa Simba ambao walikuwa wakimzomea siku za nyuma kwa madai kwamba ni mzito na hana lolote.

Katika mchezo huo wa Ngao ya Hisani uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa huku kipa wa Yanga, Deo Munishi ‘Dida’ akidaka kwa mbwembwe na sarakasi kuwakejeli Azam ambao walimtema, Jaja alipiga mabao mawili katika dakika za 56 na 65. Bao la tatu lilifungwa na Simon Msuva aliyeingia kuchukua nafasi ya Nizar Khalfan katika dakika ya 87.

No comments:

Post a Comment