Friday 3 October 2014

MUMEWA MTU SUMU HUKU KUTWA UNACHAT NAYE!

MJINI kuna maneno mengi kweli yanasemwa, kila siku linazaliwa jipya. Lakini mara zote, kinachoendelea ni kujifariji tu. Eti mara utasikia mjini hakuna wazee kila mtu baby, wapiii. Wazee wapo wengi sana, sema tu wanajitoa ufahamu.
Kati ya mambo yanayojadiliwa sana mitaani, hasa inapotokea mtu amefumaniwa ni ile kwamba mke au mume wa mtu ni sumu. Hivi ni kweli jamani ni sumu?
Moja kati ya ahadi muhimu sana ya uandishi tunayofundishwa, ni kusimamia katika ukweli, hata kama wakati mwingine unaweza kukuumiza wewe mwenyewe. Baadhi ya mambo tunajua ukweli wake, lakini labda ili tuonekane tunazingatia mila na desturi zetu, tunaukana.
Kwa mfano, tunasema mke au mume wa mtu ni sumu, hivi ni kweli tunasema kutoka moyoni? Sina uhakika, lakini tukisema Mungu atokee ghafla na kusimama mbele yetu kisha aseme ambaye hajawahi kutembea na mke au mume wa mtu atoke mbele, simuoni atakayejitokeza.
Wengi tunashiriki tendo hili ovu, ila tu inapotokea mwenzetu mmoja 40 zake zimefika, ndipo tunasema mke au mme wa mtu sumu. Juzikati nilikutana na dada mmoja aliyeomba nimshauri kidogo kuhusu jinsi anavyotakiwa aishi na mpenzi wake.
Lakini kadiri tulivyokuwa tukizungumza, hatimaye nikabaini kwamba kumbe mpenzi anayemzunguzia, ni mume wa mtu. Ni binti wa miaka 20 na mwenzake ana miaka 50, baba wa familia yenye watoto wanne.
Msichana anaonekana amekufa kwelikweli kwa huyo mbaba, maana anataka naye awe analala nyumbani kwake, walau mara mbili kwa wiki, kitu ambacho mwanaume anakipinga, yeye hataki kulala nje ya mke wake, lakini yupo tayari kuwa naye kila wakati mchana kutwa.
“Yaani huyu baba jamani, natamani tu niwe nachat naye kila saa, nampenda sana. Najua ni mume wa mtu, lakini nampenda, siamini wanaosema mume wa mtu sumu, mbona huyu baba mtamu sana?”
Huyu dada ni mmoja kati ya maelfu wanaotembea na wanawake au wanaume wa wenzao. Uzoefu unaonyesha kuwa ni wanandoa wachache wanaoficha kuwepo katika uhusiano.
“Mke wako akijua je, wee mi naogopa kupigwa” ni maneno yao akina dada wanapotongozwa na waume za watu. Ingawa hujichelewesha, lakini mwisho wa siku hukubali kuwa katika uhusiano.
Unamkuta mtu yuko bize na simu, anachat na aliyemsevu kwa jina la Baby, ukimfuatilia, ni mume wa mwenzie!Hata wanaume, wanajua kabisa huyu binti anayemmezea mate ni mke wa mtu, lakini kwa makusudi anampa majaribu, anamkaribisha lunch, kumtoa out, anampeleka shopping na vitu chungu nzima za ulaghai, mwisho wa siku wanafanya kile ambacho wenyewe wanasema ‘tunaiba’.
Kama tutafanya sensa sasa hivi, tutagundua kwamba asilimia kubwa ya wasichana tunaopishana nao mitaani, wanatoka na waume za watu, lakini wakiona fumanizi la mwenzao, wanasema mume wa mtu sumu.
Pamoja na ukweli huu kuwa mchungu, lakini bado inawezekana sana kujihadhari na wake au waume wa watu kwa sababu kama tunavyoshuhudia mara zote, ni hatari sana. Tunawaona wanaume wanaokutwa wanavyofanyiwa unyama na wengine hata kutolewa roho.
Tatizo ni kubwa zaidi kwa wasichana wanaosema kuwa ni afadhali ya kuwa na wapenzi watu wazima kuliko vijana wenzao, kwani siyo waaminifu katika uhusiano wao. Kwa hiyo wanaona hata kama atakuwa ni mume wa mtu, lakini angalau anamuondolea stress na kumpa mahitaji yake muhimu ya maisha.

No comments:

Post a Comment