Monday 20 October 2014

MBEYA::WALIMU MBEYA WAMUUNGA MKONO LOWASSA


NA GORDON KALULUNGA, MBEYA
WALIMU wa wilaya ya Mbeya, Jimbo la Mbeya Vijijini, wameunga mkono sera isiyo rasmi ambayo imewahi kutolewa hivi karibuni na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kuwa kipaumbele cha Serikali kiwe Elimu kwanza badala ya kilimo kwanza.
Hayo yameelezwa jana na Mwenyekiti wa Chama cha walimu wilaya ya Mbeya, Anthony Mwaselela, alipokuwa akisoma risala ya walimu katika maadhimisho ya siku ya walimu duniani-Wilaya ya Mbeya yaliyofanyika katika tarafa ya Isangati, kata ya Ilembo, mbele ya mgeni rasmi Prof. Norman Sigalla.
Mwaselela alisema kuwa, kutokana na serikali kutoweza kuwekeza kikamilifu katika elimu, walimu kwa sasa wanachopata na kukifurahia kwa taaluma yao ni neno Shikamoo.
“Nchi zilizowekeza kwenye elimu kwanza, ndizo zinazotisha kimaendeleo duniani mfamo China, hata sisi tunaweza kutoa tamko maana hatujachelewa, twaweza kimbia, elimu kwanza badala ya kilimo kwanza” alisema Mwalimu Mwaselela.
Alisema katika wilaya ya Mbeya inakabiliwa na changamoto nyingi zinazotokana na kutowekeza katika elimu, ikiwemo suala la nyumba za walimu, madawati, ofisi za walimu, vyoo, madai ya fedha za likizo, kuchelewa kupanda madaraja hasa kwa walimu wanaojiendeleza na malimbikizo
Kuhusu nyumba za walimu alisema mahitaji ni nyumba 1906, zilizopo ni nyumba 477 nazo zina hali mbaya, mahitaji ya vyoo vya walimu ni matundu 373, yaliyopo ni matundu 267 yenye hali mbaya na madawati mahitaji ni 21931, yaliyopo ni 17328 lakini nayo yana viraka.
“Hali hii inatokana na kutowekeza katika elimu. Kutojipanga vizuri kwa serikali upande wa elimu kiuwekezaji, kumesababisha walimu wengi kuwa na kero nyingi zinazowavunja moyo kiutendaji na hata kuwafanya vijana wengi kutopenda kazi ya ualimu pamoja na kuwa na heshima nyingi za Shikamoo”alisema Mwaselela.
Akijibu risala ya walimu hao, Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Prof. Norman Sigalla, alisema kitaalamu mwalimu bora zaidi ni yule wa shule ya Msingi akifuatiwa na mwalimu wa Sekondari.
Alisema changamoto za walimu walizosema mbele yake ni halali lakini tatizo ni uwoga wa walimu kueleza kero zao kwa viongozi wanaohusika, ambapo kwa wilaya hiyo, asilimia 90 ya walimu hawajawahi kufikisha malalamiko yao kwa Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya ambaye ni mwajiri wao na kiongozi wa serikali ambaye ni yeye Mkuu wa wilaya.
Akielezea tatizo la walimu kutopandishwa madaraja kwa wakati alisema kuwa, tatizo siyo la kimfumo kama walimu wanavyotafsiri, bali ni kutotimiza wajibu wa baadhi ya watumishi wanaohusika katika suala hilo na bahati mbaya walimu wananungunika badala ya kufikisha malalamiko yao kwa viongozi wa serikali hasa ofisi za wakuu wa wilaya.
“Nisisitize kwenu walimu wenzangu kuwa, serikali yenu ya CCM, ina lengo zuri, bali wakosaji wengi wa utumishi wa umma wanapokosea wanasingizia wegine. Wakiwazungusha na kuwajibu kwa dharau, njoo ofisini kwangu, maana Mkuu wa wilaya ndiye mwenye serikali”alisema mkuu huyo wa wilaya.
Alisema katika ofisi yake anapokea walevi, wavuta bangi na watu kadha wa kadha kwa ajili ya kusikiliza hoja wala siyo ulevi au uchafu wa mwonekano wa mtu, na akahoji sembuse Mwalimu?

baada ya hotuba yake, aliendesha harambee ya kuchangia madawati ya shule za msingi za tarafa hiyo ambapo zilipatikana Milioni Shilingi sita.

No comments:

Post a Comment