CAPT. SHITAMBALA APANDISHWA KIZIMBANI
Wakili Capt. Sambwee Shitambala(kushoto) akijadiliana na wakili anayemtetea Luambano nje ya mahakama leo asubuhi. |
Wakili na
mwanasiasa machachari Mkoani Mbeya, Capt. Sambwee Shitambala,
amepandishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi mfawidhi wilaya ya Mbeya
leo, baada ya mfanyabiashara raia wa Kiasia Jaswinder
Palsingh mkazi wa Jijini Mbeya kumtuhumu.
Wakili wa serikali Ahmed Stambuli, mbele ya Hakimu mkazi wa Wilaya ya Mbeya Gilbert Ndeuruo, alisema kuwa mshitakiwa anakabiliwa na kosa moja la kuingia kwa
jinai kinyume cha sheria namba 79 ya mwaka 2014 kinyume cha kanuni namba
16 za
sheria ya adhabu. Alisema
Shitambala anadaiwa kumfanyia maudhi Singasinga huyo kwa kuingia kwa
jinai na kujenga katika viwanja namba 27 na 28 Kitalu BB vilivyopo eneo
la Gombe Uyole jijini Mbeya ambavyo vinadaiwa kuwa ni mali halali ya
Kalasinga huyo.
Shitambala
ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM(mnec) kupitia wilaya ya Mbeya mjini, amedaiwa kufanya
kosa hilo kati ya Juni, 18 2012 na Novemba 28,2013.
Mara baada
ya kusomewa shitaka hilo, mshitakiwa ambaye alikuwa akitetewa na wakili wa
kujitegemea Tasco Luambano alikana shitaka hilo ambapo hakimu Ndeuruo alisema
kuwa dhamana ya mshitakiwa iko wazi na anaweza kuwa nje kwa dhamana iwapo atatimiza masharti ya kuwa
na mdhamini mmoja na ahadi ya fedha sh. milioni 1.
Mshitakiwa
ambaye hakuwa na mdhamini aliruhusiwa kujidhamini mwenyewe kwa ahadi ya fedha
sh. milioni 1.
Hakimu
Ndeuruo aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 10 ambapo itaanza kusikilizwa
rasmi.
Akizungumza
nje ya mahakama wakili anayemtetea Shitambala, Luambano alisema kuwa mteja anawakilisha
wakazi wengine 400 ambao wamejenga pamoja naye katika eneo hilo na kuwa hata
hivyo ameshitakiwa yeye peke yake.
Aidha
washitakiwa wengine wanne ambao walikamatwa pamoja na Shitambala na kufika
mahakamani hapo hawakuhusishwa na kesi hiyo na kutakiwa kukaa pembeni kwa kuwa
kesi hiyo haikuwahusu wao.
Waliokuwa pamoja na
Shitambala mahakamani hapo ambao waliwekwa pembeni kwa madai kesi hiyo
haiwahusu ingawa walikamatwa na polisi na kufikishwa kituo cha polisi
cha Kati Jijini Mbeya, hapo ni pamoja na Jane Kamage, Hilda
Ngowi,Clavery Mayangu na Said Mpunga.