AMA kweli fedha mwanaharamu! Kama bado ulikuwa ukiamini kwamba Beautiful
Onyinye, Wema Isaac Sepetu anayependelea kuitwa Madam ana mtonyo
(fedha) kumzidi aliyekuwa shosti wake, mwigizaji Kajala Masanja ‘Kay’,
umekosea sana kwani upepo umegeuka, ungana na Ijumaa Wikienda. Habari za
‘ufukunyuku’ zinadai kwamba, kwa utajiri alionao kwa sasa, Kajala
anaweza kudiriki kumwajiri Wema kama kisemavyo chanzo.
TUJIUNGE NA CHANZO Kwa mujibu wa chanzo makini kilicho karibu na wote
kwa maana ya kutafuna pande zote, mwigizaji huyo ambaye enzi za ushosti
wake na Wema alikuwa akionekana kama kijakazi, sasa fedha imemtembelea
kiasi cha kutosha wakati mwenzake kwa bahati mbaya eti ‘anatembelea
ringi’. Chanzo kilisema kwamba Kajala kwa sasa ana maisha ya ‘kitonga’,
amepanga kwenye nyumba nzuri ya ghorofa, ana kampuni yake ya filamu (KAY
Entertainment), magari manne, anatembea na wapambe (walinzi) huku
akaunti yake benki ikiwa imetuna. “Kajala ameonesha jeuri ya fedha.
Ametoka katika nyumba ya kawaida sasa analala angani. Kwa taarifa yenu
amepanga ghorofa nzima maeneo ya Sinza-Madukani jijini Dar. “Yupo
vizuri, anamiliki ofisi kubwa ya kuzalisha sinema, magari mawili ya
ofisi pamoja na magari mawili ya kutembelea (Brevis na Harrier) na
anaishi katika nyumba anayolipa kodi kwa mwezi dola 2,000 (zaidi ya Sh.
milioni 3.2),” kilidai chanzo hicho na kudai kwamba si mbaya Kajala
akamkumbuka mwenzake hata kwa kumwajiri kwenye kampuni yake.
KAJALA AMEHONGWA? Akizungumza na waandishi wetu, Kajala alisema
anamshukuru Mungu kwani fedha hizo amezizalisha kupitia kazi zake pamoja
na biashara mbalimbali alizokuwa akizifanya, hajahongwa na mtu yeyote.
“Sijahongwa na mtu yeyote, kila mtu ana akili zake katika kutafuta
fedha, nafanya biashara huku nikiigiza sinema zangu na Mungu amenijalia
mambo yanakwenda vizuri,” alisema Kajala. Kuhusu kumwajiri staa mwezake
huyo, Kajala hakutaka kulizungumzia hilo. WEMA HALI IPOJE? Utafiti
uliofanywa na Ijumaa Wikienda umebaini kwamba Wema aliyemlipia Kajala
Sh. milioni 13 asiende jela mwaka jana, ambaye kipindi kifupi
kilichopita alikuwa na kampuni ya kuzalisha sinema, wapambe, akaunti
iliyonona benki, magari ya kifahari ya kutembelea na samani nyingine,
nyingi zimepotea kama si kuyeyuka kabisa.
Utafiti umeonesha Wema ambaye alikuwa akimiliki magari kadhaa likiwemo
la kufanyia kazi za sinema, kwa sasa amebakiwa na gari moja tu ambalo ni
Toyota Harrier. Kama hiyo haitoshi, ilidaiwa kuwa hata akaunti benki
haijanona na hata wapambe wa kutembea naye wameyeyuka. WEMA ATAFUTWA Ili
kutaka kujua anazungumziaje ‘challenge’ hiyo ya kudaiwa kuporomoka
kiuchumi, wanahabari wetu walimtafuta Wema kwa siku tatu mfululizo
lakini hakupatikana huku simu yake ikiita muda mrefu bila kupokelewa.
SHOSTI WAKE Akizungumza na waandishi wetu kwa sharti la kutoanika jina
gazetini, rafiki wa karibu wa Wema alikiri kuwa staa huyo mwenye nyota
isiyochuja, ameshuka kiuchumi tofauti na enzi zile ambazo walikuwa
wakitanua katika viunga mbalimbali na msururu wa watu huku Madam
akisimamia shoo nzima ya malipo. “Madam kwa sasa ameshuka kiuchumi kwani
hatutanui mjini kama ilivyokuwa zamani, yaani naamini anaweza kuajiriwa
na Kajala ambaye wakati ule alikuwa chini kwake,” alisema rafiki huyo.
KUMBUKUMBU YA JUZIKATI Hivi karibuni, baadhi ya mashabiki wa Wema ambao
wanajiita Team Wema, walimuonya staa wao huyo wakidai ananyonywa na
mpenzi wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye pia amekuwa
akimdhalilisha katika majukwaa pindi anapofanya shoo zake. Walimtaka
abadilike kwani yeye ndiye mwenye nyota ya kung’aa lakini Diamond
ananufaika yeye peke yake na muziki wake. DIAMOND ALINENA Baada ya
Diamond kushambuliwa na Team Wema, naye alitoa majibu ambayo yalionesha
dhahiri kwamba ndiyo sababu inayomfanya Wema ashuke kisanaa na kiuchumi.
“Kama kweli mnampenda huyo msanii wenu (Wema) basi mngemshauri kwanza
akaacha kufanya starehe kuliko kuelekeza lawama kwangu, mimi kama mume,
jukumu langu ni kuhakikisha namwezesha kuanzisha biashara lakini jukumu
la kuendeleza ni la kwake, mnataka hata kuigiza nikamuigizie?,” alihoji
Diamond mtandaoni.
No comments:
Post a Comment