Mwenyekiti
wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ‘amekomaa’ kuhakikisha Bunge
Maalumu la Katiba linafanya kazi kwa kasi na kukamilisha kila kitu
ifikapo tarehe yake ya mwisho, Oktoba 4, ikiwamo kupiga kura za
kupitisha Katiba inayopendekezwa kazi ambayo amesema itafanywa hadi nje
ya nchi kwa wajumbe watakaokuwa huko.
Sitta
alilazimika kutoa matamko mawili kwa nyakati tofauti, mara ya kwanza
wakati kikao cha Bunge kilipoanza jana akieleza jinsi Rasimu ya Katiba
inayopendekezwa itakavyokamilika ifikapo Septemba 21 na baadaye mchana
wakati akiahirisha Bunge alipotangaza mikakati ya kukusanya kura za
wajumbe hadi nje ya nchi kuanzia Septemba 26, mwaka huu.
Sitta
alitumia fursa hiyo kuwataka wajumbe wa Bunge hilo watakaokuwa nje ya
nchi kwa matibabu au sababu nyingine kuacha mawasiliano yao ili waweze
kupiga kura wakiwa hukohuko.
Alisema
uongozi wa Bunge umeanza kufanya mawasiliano na balozi mbalimbali za
Tanzania nje ya nchi ili wawepo watumishi wake watakaokula kiapo cha
kisheria ili wasimamie upigaji kura.
Kauli
za Sitta zimekuja siku moja baada ya Kituo cha Demokrasia Tanzania
(TCD) kuweka bayana makubaliano baina ya wajumbe wake na Rais Jakaya
Kikwete kuwa hataongeza muda wa uhai wa Bunge hilo, hivyo litakoma
Oktoba 4, mwaka huu na hakutakuwa na upigaji wa kura ya maoni kupitisha
Katiba hiyo hadi baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 2015.
Kauli za Sitta
Akizungumza
bungeni kwa kujiamini lakini bila kugusia ratiba ya Bunge hilo
iliyokuwa inafikia Oktoba 30, mwaka huu, Sitta alisema ratiba ya Bunge
hilo itaendelea kama tangazo la Rais katika Gazeti la Serikali
linavyosema.
GN
hiyo namba 254 iliyotolewa Agosti Mosi, mwaka huu, ililiongezea Bunge
hilo siku 60 ambazo zinamalizika Oktoba 4, mwaka huu baada ya siku 70 za
awali kumalizika bila kupatikana katiba inayopendekezwa.
“Kwa taarifa tu na msisitizo, ni kwamba ratiba yetu ya Bunge Maalumu inaendelea kama ilivyopangwa,”alisema Sitta huku akishangiliwa kwa makofi na wajumbe waliokuwamo.
“Siku
60 za Bunge hili ambazo ni nyongeza ya siku tulizopewa na Rais kwa
mujibu wa sheria usipohesabu siku za Jumamosi, Jumapili na sikukuu,
zinaishia tarehe 4 Oktoba,” alisema Sitta.
Alisema
kikao cha Kamati ya Uongozi kilichoketi juzi, kimeelezwa kuwa Bunge
hilo linakwenda vizuri na kwamba Kamati ya Uandishi imejipanga kuwapatia
Rasimu ya Katiba Septemba 21, mwaka huu.
“Kwa hiyo ni dhahiri kabisa kwamba lengo tulilopewa na Taifa la kutoa Katiba inayopendekezwa tutalimudu ndani ya wakati,” alisema Sitta ambaye pia ni Mbunge Urambo Mashariki (CCM) na kuongeza:
“Tunaangalia
upigaji kura wa wenzetu ambao hawapo kwa sababu mbalimbali nje ya
ukumbi huu ukiacha wale waliosusa, wapo wengine wana sababu za
kutokuwapo kama vile hospitalini. Kwa hiyo itakapofika wakati wa kupiga
kura, tutatoa maelezo ya utaratibu upi utatumika kuweza kuwapata hao kwa
sababu akidi inahusu sisi sote ambao tuliteuliwa na Mheshimiwa Rais.”
Kwa
mujibu wa tafsiri ya Kanuni za Bunge, “Akidi” maana yake ni idadi ya
wajumbe inayoruhusiwa kwa madhumuni ya kuanza kikao cha Bunge Maalumu,
Kamati au kufanya uamuzi wa Bunge Maalumu au wa Kamati ya Bunge Maalumu.
Sitta
alitangaza pia kuwa mjadala ambao ulianza Jumanne iliyopita ungeendelea
hadi keshokutwa, tofauti na tangazo lililotolewa awali na Makamu
Mwenyekiti wake, Samia Suluhu Hassan kuwa majadiliano yangechukua siku
nane hadi Alhamisi ijayo.
Ili
kukamilisha dhamira hiyo, Jumamosi imerudishwa kuwa siku ya kazi, licha
ya awali kuondolewa pamoja na siku za Jumapili na sikukuu na kuzifanya
za kazi kinyume na utaratibu uliokuwa umezifuta kwa kuzingatia “sheria
za kazi.”
Baadaye,
kabla ya kusitisha shughuli za Bunge mchana, Sitta alitoa tangazo
jingine, akibainisha kuwa upigaji kura utaanza Septemba 26 na utafanyika
hata kwa wajumbe watakaokuwa nje ya nchi.
Sitta
alikuwa akitoa tangazo hilo kurejea maombi ya baadhi ya wajumbe wa
Bunge hilo ambao ni waumini wa Kiislamu wanaopanga kwenda Hija kuanzia
Septemba 22, mwaka huu.
Lukuvi ajiweka kando
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi
alipoulizwa jana iwapo anadhani siku zilizobaki zitatosha kumaliza
shughuli za Bunge zilizokuwa zimepangwa hadi mwisho wa Oktoba, alitaka
tamko la Sitta ndilo linukuliwe.
“Si
umemsikia mwenyekiti mwenyewe leo (jana) asubuhi akiji-commit
(akiahidi) kwamba Bunge hili litamaliza kazi yake mpaka kupatikana kwa
katiba inayopendekezwa? Unataka nini tena,” alisema.
Alipoulizwa ratiba ya awali inayokoma Oktoba 31, mwaka huu, Lukuvi alisema GN iko wazi juu ya ukomo wa Bunge hilo.
Kwa
upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema
alipoulizwa iwapo Rais ajaye atawajibika kisheria au la kuendeleza
mchakato wa Katiba pale ulipoishia alisema:
“Katiba
na sheria tuliyonayo haimbani rais ajaye kuendeleza mchakato kwa sababu
anaweza kuja na vipaumbele vyake, lakini njia pekee ya kumbana ni
kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,”alisema.
Hata
hivyo, Jaji Werema alisema wataangalia uwezekano wa kuifanyia
mabadiliko sheria hiyo ili itamke kuwa upigaji wa kura ya maoni
unaahirishwa hadi wakati wa Rais ajaye ili mchakato uendelee kuwa hai.
Hata
hivyo, pamoja na Bunge hilo kuongeza kasi ili kukamilisha kazi, taarifa
zinasema bado Katiba inayopendekezwa inaweza kukwamishwa na upatikanaji
wa theluthi mbili.
“Baadhi
ya Kamati hazikupata theluthi mbili, sidhani kama tutapata Katiba
inayopendekezwa. Angalia mawaziri na wabunge wenyewe wa CCM
hawahudhurii,” ilidokezwa.
Kigogo
mmoja wa Serikali alisema juzi kuwa ijapokuwa CCM wanajiaminisha kupata
theluthi mbili Bara na kwamba wasiwasi uko Zanzibar lakini hata bara
theluthi mbili inaweza isipatikane pia
No comments:
Post a Comment