Askofu Amos
Muhagachi akitoa tamko juu ya tuhuma mbalimbali dhidi ya kundi la 201
la wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba leo 03 Septemba, 2014 katika
Ukumbi wa Spika, Mjini Dodoma.
Mwenyekiti
wa kundi la 201 ya Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Dkt. Francis Michael
akikanusha kuhusu madai ya wajumbe wa kundi hilo kupewa rushwa kuhusu
mchakato wa Katiba Mpya.
Sheikh Hamid
Jongo akiviasa vyombo vya habari kutoa ushirikiano ili kuhakikisha
kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya unafanikiwa kwakuwa hata wao
(vyombo vya habari) unawahusu pia.
Askofu
Donald Mtetemela akichangia mada wakati wa mkutano wa kutoa tamko
kuhusiana na tuhuma mbalimbali dhidi ya kundi la 201.
Baadhi ya
wajumbe wa kundi la 201 pamoja na waandishi wa habari wakifuatilia
tamko hilo leo 03 Septemba, 2014 katika mkutano uliofanyika ukumbi wa
Spika Bungeni mjini Dodoma.
(Picha
zote na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma)
WAWAKILISHI
wa Taasisi za dini wa Bunge Maalum la Katiba toka wajumbe 201 wametoa
tamko lao dhidi ya tuhuma mbalimbali zinazoendelea katika kulichafua
Bunge hilo ikiwemo baadhi ya wajumbe wa kundi hilo wakituhumiwa
kudaiwa kupewa rushwa.
Tamko hilo
limetolewa leo 03 Septemba, 2014 na viongozi wa kiroho akiwemo Askofu
wa Kikristo Amos Joseph Muhagachi pamoja na Sheikh Hamid Masoud Jongo
wakiwa wameongozana na Mwenyekiti wa kundi hilo la 201, Mhe. Dkt.
Francis Michael na wajumbe wengine wa kundi hilo, wakati walipofanya
mkutano na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Spika uliopo Bungeni
mjini Dodoma.
Akisoma
tamko hilo, Askofu Amos Muhagachi ambaye pia ni Mjumbe wa kundi hilo
amesema kuwa kama ilivyoelezwa hapo awali kabla ya kuanza kwa
shughuli za Bunge hilo, kila mjumbe alikula kiapo cha kuwa mwaminifu
na mtiifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kadiri ya uwezo
wake na ufahamu wake, kufanya kazi zinazomhusu bila upendeleo.
Askofu
Muhagachi ameendelea kusema kuwa wameshangazwa na kusikitishwa kuona
kwamba mchakato wa kutayarisha Katiba itakayopendekezwa na Bunge hilo
kwa wananchi unachafuliwa taswira yake, Bunge Maalum la Katiba
linachafuliwa, shughuli zake kuingiliwa na kupotoshwa na wajumbe
wenzao walioko nje ya Bunge hilo, makundi, taasisi na vyombo
mbalimbali vya habari, uhalali na ukweli wa shughuli za Bunge hilo
unapotoshwa na wananchi wanaaminishwa mambo yasiyo na ukweli.
“Upotoshwaji
huu umezua mijadala mbalimbali katika jamii ya Watanzania bado
unaendelezwa”, alisema Muhagachi.
Aidha,
Muhagachi amezitaja baadhi ya tuhuma zinazotolewa na wajumbe wenzao
dhidi ya Bunge hilo na wajumbe wa kundi hilo zikiwemo.
“Bunge
Maalum la Katiba halina uhalali kwa kuwa hao wajumbe wenzetu
walioondoka wameliondolea uhalali wake kwa vile hawapo, kwamba Kanuni
za Bunge Maalum la Katiba zinavunjwa ovyo ovyo, Kwamba
kinachojadiliwa sasa katika Bunge hili ni Waraka mwingine na si
Rasimu iliyotayarishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Inadaiwa na
watu pamoja na Taasisi mbalimbali kwamba viongozi wa dini, wajumbe wa
Bunge hilo na wajumbe wa kundi la 201 kwamba wanapewa rushwa baadhi
ya Vyombo vya Habari vimeandika tuhuma hizi, pia madai mengine ni
kwamba wajumbe waliomo katika Bunge hili ni wachache ikilinganishwa
na hao waliopo nje ya Bunge na tuhuma ya nyingine ni ile ya kwamba
Bunge hili lazima lisitishwe au livunjwe na Mhe. Rais.
“Tunapenda
kuwafahamisha Watanzania wenzetu kwamba mchakato wa Katiba una hatua
tatu kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na mpaka hivi sasa
ni hatua moja iliyokamilika, aidha hatua ya pili ndiyo inayoendelea
na hatua ya tatu bado haijaanza”, alisema Muhagachi.
Akitoa tamko
hilo, Askofu Muhagachi amesema kuwa wao kama wawakilishi wa Taasisi
za Dini, ambao kuuhubiri, kuutangaza na kuusimamia ukweli ni moja ya
majukumu yao katika jamii, hivyo wameskitishwa na taarifa potofu
zinazosambazwa kwa makusudi na makundi, taasisi na baadhi ya vyombo
vya habari.
“Tukiwa
kama wajumbe wa Bunge hili ambao tunafahamu kwa kina na tunaridhika
na kila hatua ya mchakato huu, tuna wajibu wa kusahihisha upotofu huu
unaoendeshwa kwa makusudi na hivi kuwaeleza Watanzania ukweli na hali
halisi inayojiri hapa Bungeni, Watanzania msifadhaishwe na wala
msibabaishwe, hali ni shwari, mchakato unaendelea kwa amani na
utulivu”, alisisitiza Muhagachi.
Naye Sheikh
Hamid Masoud Jongo ameviasa vyombo vya habari kutilia mkazo katika
kutoa taarifa zilizosahihi ili mchakato wa Katiba uendelee kwa amani
kwani nao ni moja ya kundi la watu inayowahusu.
“Vyombo
vya habari vina nguvu ya kuhabarisha umma juu ya mambo mengi
yanayoendelea nchini, ni vema tukishirikiana sote kwa pamoja ili
kuhakikisha kuwa tunapata Katiba yetu kwani hata nyie Katiba hii
inawahusu hasa katika kudai haki na uhuru wa vyombo vya habari”,
alisema Sheikh Jongo.
Aidha,
Mwenyekiti wa wajumbe wa Kundi hilo la 201, Mhe. Dkt. Francis Michael
ameongezea kwa kukanusha suala la rushwa kwa wajumbe wake huku
akisisitiza kuwa wajumbe wake katika kundi hilo ni watu wenye heshima
zao hivyo madai hayo hayana ukweli wowote ule.
No comments:
Post a Comment