Je,
upo kwenye uhusiano wa kimapenzi, unampenda sana mume, mke, mchumba au
mpenzi uliyenaye lakini wazazi au ndugu zako wanamchukia na kila siku
wanampiga vita?
Mada ya leo ni kwa ajili ya wewe msomaji wangu ambaye upo kwenye
mazingira kama haya ya wazazi au ndugu kumkataa umpendaye kwa sababu
ambazo wanazijua leo. Kwa ambao wamewahi kupitia changamoto hii au bado
wapo ndani yake, watakuwa wanaelewa vizuri ugumu uliopo linapokuja suala
kama hili.
Wazazi wako wamekuzaa na kukulea tangu ukiwa mdogo mpaka umekuwa
mkubwa, umempata umpendaye lakini wao wanamkataa na kukwambia unatakiwa
kuchagua moja, wao (wazazi) au huyo unayempenda. Utachukua uamuzi gani?
Utamuacha kwa sababu wazazi hawampendi? Utakubali kuwadharau wazazi wako
na kuendelea naye?
Bila shaka kila mmoja atakuwa na jibu lake tofauti, hata mimi
ukiniuliza nitakuwa na jibu langu lakini tunachokihitaji hapa, ni
kujadiliana, kupanuana mawazo, kupeana uzoefu ili mwisho kila mmoja awe
na uwezo wa kuivuka changamoto hii kwa sababu hata kama bado
haijakukuta, huenda ipo siku na wewe yatakutokea.
MFANO HAI
Hebu soma ushuhuda wa msomaji wangu mmoja ambaye yupo kwenye hali mbaya na anahitaji ushauri:
“Mimi ni mwanaume mwenye umri wa miaka 42, nilioa miaka kumi iliyopita
na tumejaliwa kupata watoto wawili. Tatizo linalonisumbua na kuniweka
njia panda, mke wangu anawachukia sana wazazi wangu na ndugu wote kutoka
upande wangu.“Wazazi
wangu wamekuja mjini kwa zaidi ya miezi miwili sasa kwa ajili ya
matibabu lakini huwezi kuamini, mke wangu anawachukia kiasi kwamba hata
salamu kwake ni mtihani. Anawadharau, wanapishana ndani kama wake wenza,
anazungumza maneno machafu dhidi yao ambayo mengine nayasikia, hawapi
matunzo mazuri, anawanyanyasa na kibaya anawafundisha mpaka wanangu
kuwadharau babu na bibi.
“Hali hiyo imesababisha wazazi nao waanze kumchukia sana, wananiambia
nimekosea kuchagua mke na wananitolea maneno makali ambayo mengine
hayaandikiki. Nipo njia panda, sijui niamue nini, bado nampenda mke
wangu lakini mambo anayoyafanya yamesababisha mapenzi yangu kwake
yapungue mpaka nafikiria kumpa talaka ili kuwafurahisha wazazi wangu.
Naomba ushauri, nifanyeje?”
Amehitimisha msomaji wangu huyu, bila shaka umemuelewa. Najua huyu ni
mmoja tu lakini wapo wengi ambao wanatokewa na visa kama hivi. Naomba
tujadiliane pamoja, ungekuwa ni wewe kwenye nafasi ya msomaji huyu,
ungefanya nini? Kama ungepewa kazi ya kumshauri, ungemwambia nini?
TAFUTA CHANZO CHA TATIZO
Hakuna chuki ambayo
huwa haina chanzo. Kama mumeo, mkeo anawachukia ndugu zako, jambo la
kwanza ambalo unatakiwa kulijua, ni kwamba lazima kuna chanzo
kilichosababisha hali hiyo. Na kama yalivyo matatizo mengine yote,
huwezi kupata muafaka kama hujakijua chanzo.
Wengi hushindwa kutumia busara katika kutafuta chanzo. Yawezekana
umpendaye ndiyo chanzo ila kwa sababu ya mapenzi yako kwake, unaukataa
ukweli na kumtetea.
No comments:
Post a Comment