NA GORDON
KALULUNGA
WIKI hii ni
wiki ya Vijana, Rais Jakaya Kikwete, wakati anazima mwenge wa uhuru mkoani
Tabora mwanzoni mwa wiki na kumbukumbu ya miaka 15 ya kifo cha Mwalimu Julius
Nyerere, alisema vijana ndiyo wanufaika wakubwa na Tanzania ijayo.
Katibu Mkuu
wa CCM Taifa, Abdulhaman Kinana, akiwa mjini Dodoma wakati wa semina za
makatibu wa CCM nchi nzima katikati ya wiki hii, amewaambia kuwa katika ngazi
zao za uteuzi wawe makini kupendekeza majina ya watu wanaokubalika na jamii
badala ya fedha.
Ukitaka kuwaudhi
baadhi ya viongozi wa CCM, ambao wamezoea kufikiri kidogo badala ya kufikiri
sana, waulize swali la kwanini majimbo ya upinzani yanaongezeka.
Wanaishia
kusema kuwa ni kutokana na makundi ndani ya chama, badala ya uhalisia kuwa
rushwa katika ngazi za uteuzi imetawala, hivyo watu wanaokubalika katika jamii
wasio na fedha huachwa.
Leo sauti ya
nyikani inatokea mkoni Mbeya na kuangaza upepo wa kisiasa uliopo jimbo la Mbeya
mjini.
Kwa sasa
Jimbo la Mbeya Mjini lipo chini ya Chama cha demokrasia na Maendeleo(Chadema),
na Mbunge wake ni Joseph Mbilinyi.
Mbunge huyu
amekuwa akipongezwa na baadhi ya wananchi kuwaletea maendeleo katika kata zao
kwa kile wachambuzi wa masuala ya siasa mkoani hapa wakisema anatumia vema hasa
usimamizi mzuri wa matumizi ya fedha za mfuko wa Jimbo.
CCM, inahaha
kulirejesha jimbo hilo katika himaya yake, lakini kitendawili kinabaki miongozi
mwao kuwa ni nani mwenye kuwaunganisha wote, ukizingatia kuwa asilimia sabini
ya wajumbe wa kamati ya siasa ambayo ni kikao cha maamuzi kwa watakaohitaji
kugombea nafasi hiyo nao wanatajwa kuwemo kwenye mstari wa safari hiyo ya
matumaini.
Baadhi ya
watu wanaotajwa kuwemo katika kinyanganyilo hicho cha ubunge nje ya kamati ya
siasa ya CCM wilaya ya Mbeya mjini ni pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la nyumba
Tanzania(NHC), Nehemiah Mchechu, Mwenyekiti wa saccos kubwa Jijini Mbeya, (UWAMU
SACCOS), Rodrick Y. Nyaluke na mjasiliamali kijana, Nwaka Mwakisu.
Wengine ni
Mkuu wa wilaya ya Newala, Christopher Magala na Mtaalamu wa Masuala ya
Ufuatiliaji na Tathimini, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (OWM – TAMISEMI), Eliurd Leonard Mwaiteleke.
Leo nikianza
na kijana Eliurd Mwaiteleke, anatajwa katika mbio hizo za kuweza kupeperusha
bendera za CCM katika jimbo hilo la Mbeya Mjini kwa nia ya kukomboa jimbo, huku
baadhi ya vijana wakimpa ‘‘dole’’, ukizingatia kuwa ni kamanda wa UVCCM kata ya
Sinde Jijini Mbeya na alipendekezwa kuwa kamanda wa UVCCM mkoa wa Mbeya,
akuweza kufanikiwa kutokana na umri wake.
Kabla
sijaandika makala haya, nilijaribu kumtafuta na kutaka kujua wasifu wake, mbali
na kukataa kuwa ni mmoja wa waliotangaza nia katika jimbo hilo, alisema kuwa
yeye ni mtoto wa masikini lakini jitihada zake zimemfikisha hapo alipo.
Mwaiteleke alizaliwa
May 28, 1977, eneo la Mwanjelwa jijini
Mbeya, mwaka 1986 alipelekwa kujiunga na shule ya Msingi Salemu, wilayani
Rungwe mkoani Mbeya na kuhitimu mwaka 1992, kisha akajiunga na shule ya
sekondari Ivumwe Jijini Mbeya kati ya mwaka 1993-1996 na mwaka 1997 na 1999
akajiunga na kidato cha tano na sita shule ya Sekondari Malangali
Kijana huyu, anasema kwa sasa ana elimu ya Shahada
ya Uzamili katika Sayansi ya Maendeleo ya Sera (Master Degree of Science in
Development Policy (MSc.DP), aliyotunukiwa katika Chuo Kikuu Mzumbe, baada ya
kusoma tangu mwaka 2009 – 2011, akitokea Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini
(Institute of Rural Development Planning - Dodoma (IRDP) baada ya kuwa na cheti
na stashahada ya juu katika masuala ya mipango na mazingira.
Kijana huyu
pia ni mtaalam wa masuala ya Ukusanyaji Takwimu Muhimu za usafi wa Mazingira, mtambuzi
wa walengwa wa njaa na ugawaji wa
chakula na mwibuaji na msimamizi wa miradi ya kijamii kwa jamii iliyoathirika
na UKIMWI.
Mwaiteleke
anaonesha hulka na akipendacho kuhusu mipango na masuala mengine muhimu ya mwelekeo wake kuwa ni kuungana na vijana wenzake
kusaidiana mambo ya maendeleo kwa kutumia ujuzi na elimu aliyonayo hasa
kuelezana kuhusu fursa zilizopo, changamoto na namna ya kuzifikia pamoja na
kuzitatua ili wapate maendeleo yanayotarajiwa.
Kuhusu
heshima ya Mbeya anasema, ni vema vijana wa mkoa wa Mbeya, wakatambua namna
wazee wao jinsi walivyojenga heshima ya Mkoa wa Mbeya na namna wao wanavyoweza
kusaidia kurudisha heshima na hadhi ya Mbeya inayopotea siku hadi siku.
Anaamini
katika juhudi kwa kila jambo ili kuweza kuleta tofauti katika maisha ya jamii
nzima ya wana Mbeya, ikiwa ni pamoja na kuanzisha mijadala ya wazi kwa vijana
katika Nyanja mbalimbali.
Nyanja
ambazo anazipa kipaumbele katika mijadala ni pamoja na masuala ya maendeleo ya
elimu (tathimini ya elimu katika mkoa), afya, Mazingira na usafi wa Jiji la
Mbeya, ukuzaji kipato cha jiji na kuwafikia wananchi, Miradi ya maendeleo,
fursa za mikopo kwa vijana na wanawake na namna ya kuzikifikia.
“Tulikuwa na
viwanda Jijini Mbeya, leo hii vimepungua, ni suala ambalo pia linahitaji
mijadala kwa ajili ya kujua namna vinavyoweza kutengeneza ajira kwa vijana, kuanisha
mapungufu yanayokwamisha maendeleo ya Mkoa na Kuanisha mapungufu na changamoto
zinazowakabili vijana” anasema Mwaiteleke.
Anasema
angependa vijana wawe na mwanga wa kutambua masuala ya jiji , uwajibikaji wake
pamoja na ubunifu wa kiutendaji, kujua kufanya mapitio ya mipango inayopangwa
kila mwaka kama inaleta tija kwa kundi kubwa la vijana ama la.
Kwa upande
wa mtazamo wake kuhusu wazee anasema ni muhimu kutambua mahitaji halisi ya
wazee na vipaumbele vyao na jinsi ya kuwatekelezea mahitaji yao bila kusahau
masuala ya akina mama na vipaumbele vyao.
Hasiti kueleza
kuhusu masuala mtambuka ya VVU, kilimo na fursa ya kilimo cha maua kwa vijana
hasa ukizingatia fursa ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe na fursa za
wasomi waliopo na wajasiliamali.
Huyu ndiye
kijana Eliurd Mwaiteleke, ambaye anatajwa kuwa na nia ya kuipeperusha bendera
ya CCM katika Jimbo la Mbeya Mjini kwa lengo la kulikomboa Jimbo kutoka
mikononi mwa Chadema.
Wiki ijayo
tutamwangalia kijana mjasiliamali na mpenda michezo kwa vijana wenzake Nwaka
Mwakisu.
No comments:
Post a Comment