Friday 10 October 2014

SIASA::PROFESA BAREGU AFICHUA SIRI NZITO TUME YA KATIBA


Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu

Aliyekuwa  mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu, ametoboa siri kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Joseph Warioba alikuwa na msimamo wa serikali mbili, kabla ya tume kuja na rasimu yenye muundo wa muungano wa serikali tatu uliotokana na maoni ya wananchi walio wengi.


Baregu alitoboa siri hiyo wakati akizungumza na NIPASHE katika mahojiano maalum yaliyofanyika nyumbani kwake mwanzoni mwa wiki hii. Alikuwa akijibu moja ya maswali aliyoulizwa kuhusiana na namna wao (tume) walivyoondosha tofauti za kimtazamo miongoni mwa wajumbe na kuandaa rasimu iliyokubaliwa na wajumbe wote; tofauti na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ambayo walitofautiana sana kuhusiana na suala la muundo wa muungano na mwishowe, wajumbe wengi wa upinzani wakasusia vikao kupitia mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kuwaachia wenzao wanaoundwa na wafuasi wengi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuendelea na kazi hiyo.

Wajumbe wanaounda Ukawa ambao wengi ni kutoka vyama vikuu vya upinzani nchini vya NCCR-Mageuzi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF) walisusia vikao vya Bunge la Katiba kutokana na madai yao kuwa rasimu iliyoandaliwa na tume iliyoongozwa na Warioba kwa kuzingatia maoni ya wananchi ilibadilishwa kwa maslahi ya CCM. Ukawa walikuwa wakitetea rasimu ya Warioba iliyopendekeza muundo wa muungano wa serikali tatu huku wajumbe wengi wa CCM wakisisitiza kuwa na muundo wa muungano wa serikali mbili lakini ulioboreshwa. 

Akieleza zaidi, Baregu alisema kuwa kwa ujumla, tume ilijigawa kwenye kamati ndogo tatu wakati wa kuanza kujadili mapendekezo, ambazo ni kamati ya mihimili ya utawala (bunge, serikali na mahakama), kamati ya iliyokuwa ikishughulikia misingi na maadili ya taifa na kamati ya tatu ndiyo iliyokuwa ikishughulikia masuala ya muungano.

“Labda niwaeleze tu, hiyo kamati ya muungano tuliipa jina kama kundi la kifo... na ninalitaja kundi hili kwa masikitiko kwa sababu mmoja wetu, Dk. Mvungi alifariki kweli,” alisema.

Prof. Baregu alisema kundi la kifo lilikuwa la  watu wenye misimamo kuanzia wa serikali moja, mbili, tatu  na wengine waliokuwa na mawazo ya kuwa na muungano wa mkataba.

“Akina nanihii hawa... akina Warioba, akina Butiku, Jaji August... walianza na msimamo wa serikali mbili. Mimi siku nyingi ni mtu wa serikali moja. Wakawapo watu wa serikali tatu, including (akiwamo) Dk. Mvungi. Na kundi la nne la watu wenye msimamo wa serikali ya mkataba,” alisema.

Alisema pamoja na minyukano iliyojitokeza kutokana na misimamo hiyo binafsi ya wajumbe, bado waliweza kusimama imara na kuzishinda nafsi zao kutokana na mawazo ya wananchi waliyoyapata wakati wakikusanya maoni katika maeneo mbalimbali nchini, chini ya uongozi wa mwenyekiti wao (Warioba).

Alisema kuwa awali, mwenyekiti wao (Warioba) alitoa nafasi kwa kila mjumbe kwenye suala la muungano kuzungumza na kutoa mchango wake.

“Ninakumbuka kwenye issue hii ya muungano, kila mjumbe ilibidi azungumze. Na mwenyekiti ali-insist kwamba kila mmoja wetu ni lazima achangie, na tukalizungumza kwa karibu wiki nzima,” alisema.

Prof. Baregu alisema pamoja na kila mjumbe kuzungumza, pia waliangalia maoni  waliyokusanya kutoka kwa wananchi na mwisho wa siku wakaja na maamuzi ya pamoja,  ambayo yaliwafanya kuchukua msimamo wa pamoja pia.

Alisema hawakumuacha mjumbe yeyote nyuma akiwa bado hajaridhika kwa hoja na maoni waliyokusanya na kwamba, pale ilipotokea hivyo, walianza naye kwenye kikao kilichofuata hadi kuhakikisha kwamba mhusiaka ameridhika.

“Na ndiyo maana sasa hivi ukizungumza na wajumbe wote, sijasikia hata mmoja ambaye amebadilisha mawazo, ama... au amesema kwamba alirubuniwa kwenye tume au labda kwamba Jaji Warioba alifanya maamuzi ya ubabe,” alisema.

Alisema kutokana na namna walivyoendesha mambo yao kwa uwazi na kufikia maamuzi ambayo wote waliyaafiki kikamilifu kuwa yamezingatia kwa usahihi matakwa ya wananchi, ndiyo maana bado wana mshikamano mzuri hadi sasa na wameamua kwenda kuitetea rasimu ya tume kwa wananchi.    

Amesisitiza kuwa wajumbe wa tume hiyo wamejipanga kuhakikisha wanawaelimisha wananchi kuhusu mapendekezo yaliyokuwa kwenye rasimu hiyo.

Alisema walipokuwa kwenye Tume walifanyakazi kwa bidii, weledi, nidhamu na kujenga maridhiano ndani ya jamii na ndani ya tume.

"Tuliwasikiliza wananchi wanataka nini na kuzingatia maoni ya Watanzania, na lengo la tume lilikuwa ni kupata katiba yenye maoni ya wananchi,” alisema.

KATIBA ILIYOPENDEKEZWAAlisema sasa hivi, kwenye Katiba iliyopendekezwa, kuna mambo mengi ya msingi yamenyofolewa; kama mambo ya maadili, uwajibikaji, kumwajibisha mbunge, ukomo wa ubunge, madaraka ya rais na  mawaziri kutokuwa wabunge; mambo ambayo yalipendekezwa na wananchi wengi.

Prof. Baregu alisema njia pekee ya kunusuru mchakato mzima wa katiba ni kukubali kwamba tumekwama na kukubali kusahihisha makosa badala ya kuburuza mchakato huo bila maridhiano.

Katiba iliyopendekezwa ilikabidhiwa juzi mjini Dodoma kwa marais, Jakaya Kikwete wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dk. Ali Mohamed Shein wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

“Sisi ndani ya Tume tulijenga kwanza maridhiano ndiyo maana tuliweza kutoa rasimu ambayo sote tulikubaliana,” alisema
Prof. Baregu alisema: "Kwa hali hii, ilipaswa tuwe na ujasiri wa kupumua kwanza, tukaulizana na tukakubali kwamba tumekwama kwa malengo tuliyokuwa tumejiwekea... sasa hivi ni kama mtu umepotea njia lakini unasema twende tu."

Aliongeza kuwa: "Tulikuwa na lengo, tulikuwa na ramani kwa hiyo kama tungekuwa na ujasiri kama taifa tukasema ngoja tujiulize hapa tufanye nini ili tuweze kutoka hapa, mengi tungeweza kubadilisha." Alisema mchakato umekwama baada ya kutawaliwa na wanasiasa ambao hawawezi kupitisha mapendekezo ambayo yanapingana na maslahi yao.

"Ni vyema kama tungekubali kusema hapa tumekosea, tuunde upya Bunge la Katiba, na kukubali kwamba tumekosea sana... na siyo serikali tu, lakini sote kama taifa."

Alisema. "Nimekuwa nafikiri hivi... ni kama mama mwenye mimba anayepata abortion (mimba kuharibika). Anajisikiaje?” alisema Baregu.

Alisema kwa hali ilivyopelekwa, anahisi kuwa na hali kama hiyo ya mama aliyeharibikiwa na mimba yake, kwamba amekuwa kwenye timu iliyofuatilia watu karibu mwaka mmoja na nusu kutunga katiba, lakini inaishia kusakamwa.

Alisema tume imefanya kazi kwa uadilifu, weledi

No comments:

Post a Comment