KESI KIFO CHA KANUMBA, SURA MPYA!
- Posted by GLOBAL on August 25, 2014
Stori: Shakoor Jongo
Jipya! Baada ya kimya cha muda mrefu, imefichuka
kwamba kesi ya kuuawa kwa aliyekuwa staa mkubwa wa sinema za Kibongo,
marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’ imechukua sura mpya baada ya
kuanza kusikilizwa kimyakimya, Ijumaa Wikienda limenasa kinachoendelea.
Staa wa sinema za Kibongo, Lulu Elizabeth Michael, 'Lulu".
WATU WANATAKA KUJUA KINACHOENDELEA Uchunguzi wa
gazeti hili umebaini kwamba watu wengi wana kiu ya kujua kinachoendelea
katika kesi hiyo ambapo ilidaiwa kwamba imehamishwa eneo la wazi (open)
na kusikilizwa kimyakimya katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar
es Salaam, huku usikilizwaji wa kesi hiyo ukiwa tofauti kama
ilivyozoeleka.
Kwa mujibu wa shushushu wetu anayependa kufuatilia maisha ya mastaa
wa tasnia tofautitofauti Bongo ndani ya mahakama hiyo, chombo hicho cha
kusimamia sheria kimeamua kubadili aina ya usikilizaji wa kesi hiyo.
Wakili maarufu Bongo anayemtetea 'Lulu', Peter Kibatala.
YAHAMISHIWA BARAZA LA KESI ZA MAUAJI Habari
zilieleza kwamba, kwa sasa kesi hiyo itakuwa ikisikilizwa kwenye kikao
cha baraza la kusikiliza kesi za mauaji kwenye mahakama hiyo, kwa lugha
ya kigeni kinaitwa High Court Murder Session.
“Kama ukienda pale
mahakamani ili kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo, huwezi kufanikiwa
kupata chochote kwa sababu ipo kwenye baraza la kusikiliza kesi za
mauaji yaani High Court Murder Session ambalo huwa linasikiliza kesi
kimyakimya tofauti na kesi nyingine zinazosikilizwa kwenye kizimba,”
kilisema chanzo chetu hicho.
ETI LULU HAJUI KINACHOENDELEA Uchunguzi wetu
ulibaini kwamba wakati hayo yakiendelea kortini hapo, aliyekuwa mwandani
wa Kanumba aliyekuwa naye chumbani siku ya kifo, Elizabeth Michael
‘Lulu’ hajui chochote kinachoendelea na wala hajaitwa mahakamani.
Mama mzazi wa marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa.
“Tangu imeanza kusikilizwa hakuna siku Lulu ameitwa na sidhani kama anajua kinachoendelea.
“Labda anayejua kinachoendelea ni mama Kanumba (Flora Mtegoa) ambaye
hupenda kuulizia kuhusu hatima ya mwanaye,” kilisema chanzo hicho.
WAKILI KIBATALA ANASEMAJE? Baada ya kujikusanyia
data hizo, Ijumaa Wikienda lilimtafuta wakili maarufu Bongo anayemtetea
Lulu, Peter Kibatala ili kupata ufafanuzi wa aina hiyo ya usikilizwaji
wa kesi ya mteja wake ambapo alifichua siri hiyo juu ya kesi ya kifo cha
Kanumba.
Wakili Kibatala alikiri kwamba kesi ya kifo cha Kanumba ambayo Lulu
ni mshitakiwa wa kwanza akituhumiwa kuua bila kukusudia, imebadilishwa
aina ya uitwaji huku akigoma kuingia kiundani kwani bado kesi hiyo ni
mbichi na hairuhusiwi kwa wakili kuzungumza nje ya mahakama.
Aliyekuwa staa mkubwa wa sinema za Kibongo, marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’ enzi za uhai wake.
“Ni kweli inaitwa hivyo, huyo aliyekueleza hajakosea na tunategemea
mwezi huu wa nane kikao cha baraza hilo la usikilizaji kitaendelea
lakini nisingependa kuongea sana kwani mimi siyo msemaji wa Lulu bali ni
wakili na si maadili ya kazi yangu kuzungumza nje ya mahakama. Hata
Lulu haruhusiwi kuzungumza chochote nje ya mahakama,” alisema Kibatala
aliyewahi kuwa wakili wa mwigizaji Kajala Masanja na mwanahip-hop,
Waziri Makuto ‘Lord Eyez’.
TUMGEUKIE LULU Mwanahabari wetu alipomtafuta
Lulu ili kujua kama anajua chochote juu ya kesi hiyo, mkali huyo wa
sinema za Kibongo aligoma kuzungumza chochote kama aliyoelekezwa na
wakili wake, Kibatala.
TUJIKUMBUSHE Kanumba aliyewatoa mastaa wengi wa
filamu unaowaona kwa sasa, alifariki dunia April 7, 2012 nyumbani kwake,
Vatican-Sinza jijini Dar. Kifo cha Kanumba kilidaiwa kwamba kilitokana
na kuangukia sehemu ya nyuma ya kichwa ambapo alipata mtikisiko wa
ubongo kisha kuzikwa kwenye Makaburi ya Kinondoni, Dar.