Ukweli Kuhusu Kifo cha Betty Ndejembi, Unyanyasaji Kwenye Mitandao ya Kijamii Yahusika
Ninaandika makala hii nikitambua bayana kuwa itamuudhi kila mtu
anayeingia mtandaoni kwa minajili ya kuwanyanyasa watu wengine. Lakini
siku zote ninaamini katika busara hii: kuuchukia ukweli hakuufanyi kuwa
uongo. Ukweli ni ukweli na uongo ni uongo. Ukweli hauwezi kuwa uongo, na
kadhalika uongo hauwezi kuwa ukweli. Kamwe asilani.
Wakati tunaomboleza kifo cha ndugu yetu Betty Ndejembi hatuwezi kukwepa
ukweli kwamba siku chache kabla ya kifo chake binti huyo alinynyaswa mno
kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter. Japo hadi muda huu hatuwezi
kuhusisha moja kwa moja uhusiano kati ya unyanyasaji huo na kifo cha
binti huyo, ukweli tu kwamba mtu akinyanyaswa masaa kadhaa kabla ya kifo
chake, waweza kujenga picha flani.
Naomba ieleweke kuwa simlaumu mtu kwa sababu sina mamlaka ya kufanya
hivyo bali dhima ya makala hii ni rambirambi zangu na kuzungumzia tatizo
la unyanyasaji mtandaoni, sambamba na suala zima la unafiki kila
kinapojiri kifo hususan cha mtu maarufu.
Tuna tatizo kubwa huko mitandaoni. Tumefika hatua ya kuwapa umaarufu
watu wenye matusi ya nguoni, wazushi, wambeya, wanafiki, wanaharamu na
kila aina ya binaadamu wanaostahili laana lakini twaishia kuwatukuza.
Kwa Twitter, matusi imekuwa ni njia ya mkato ya kupata umaarufu. Kuna
wenzetu wengi tu wenye 'umaarufu' huko Twitter, na ukidadisi chanzo cha
'umaarufu' huo, utaambiwa 'ah huyu ana matusi si mchezo!'
Kuna watu wazima na akili zao wanatumia muda mwingi kwenye mitandao ya
kijamii aidha kunyanyasa wenzao kama si kusherehesha unyanyasaji huo.
Marehemu aliitwa majina kadhaa ya kumdhihaki kabla ya kukutana na mauti.
Kuna waliomwita Di Maria na wanajifahamu. Japo sijui chanzo cha 'ugomvi
na aliogombana nao' (na ndio maana sikujihusisha nao kwani
haukunihusu), kuna wanafiki wengi tu waliokuwa katika nafasi nzuri ya
kuzima moto huo hasa kwa vile baadhi yao walikuwa wakizifahamu pande
zote mbili za 'ugomvi' husika.
La kukera zaidi ambalo ni wazi litajichomoza wakati wa maombolezo haya
ni unafiki: baadhi ya watu walewale waliodiriki kumwandama marehemu
wakati wa uhai wake watageuka kuwa wenye uchungu mkubwa baada ya kifo
chake. Hii inanikumbusha suala ambalo nimeshawahi kulizungumzia mara
kadhaa, katika hali ya utani japo wenye uweli, kwamba 'wakati mwafaka
kabisa wa kutafuta vipaji vya uigizaji ni kwenye misiba: watu walewale
waliokuwa wakikuchukia kwa nguvu zote watageuka wenye uchungu mkubwa kwa
kifo chako.
Ukiangalia baadhi ya tweets za mwisho za marehemu ni wazi kuwa binti huyo alikuwa anahitaji msaada kutoka kwa wanaomjali
Hata pasi uelewa wa taaluma ya saikolojia, tweets za aina hii
zinaashiria tatizo, na laiti 'wenye upendo wa dhati' wangeingilia kati
muda huo, huenda muda huu Betty asingekuwa marehemu.
Na hizo tweets mbili ambazo ni miongoni mwa za mwisho kabisa za marehemu
ni ushuhuda tosha wa jinsi alivyokuwa akisumbuliwa na wanyanyasaji
dhidi yake mtandaoni. Ndio pengine kilichomuua ni maradhi ya kawaida ya
kibinadamu lakini kila mwenye ubinadamu hatoshindwa kuhusisha
unyanyasaji huu na hali mbaya ya afya aliyokuwa nayo hadi anafariki.
Kuna watakaolaumu kuwa ninatumia kifo cha binti huyo kwa 'maslahi
binafsi.' Hapana, sina maslahi yoyote binafsi hasa ikizingatiwa kuwa
sikuwa nikifahamiana na marehemu. Hakuna anani-follow na mie sikuwa
nam-follow. Labda maslahi pekee niliyonayo ni upinzani wangu mkali dhidi
ya unyanyasaji wa mtandaoni. Vyovyote ilivyo, marehemu alikuwa bullied
kabla hajafariki na atakayetaka kukataa ukweli huo na akatae lakini
utabaki kuwa ukweli usioweza kugeuka uongo. Na kwa hakika, kila
aliyeshiriki kumnyanyasa binti huyo atakuwa anasutwa na nafsi yake, hata
kama atatafuta hifadhi kwenye 'huu sio wakati wa kulaumiana' au 'we
failed you Betty.'
Mara nyingi nimekuwa nikiwalaumu watu wanaodai 'Instagram imekuwa mbaya'
au Twitter imeharibika siku hizi' ambapo mara zote nimewakumbusha
wahusika kuwa katika hii mitandao ya kijamii, ni muhimu kuwa makini
katika nani wa kum-follow. Maana yangu ni kwamba ukim-follow mtu mwenye
matusi, utashuhudia matusi katika anachoandika. Ukim-follow mtu wa
busara, utashuhudia busara.
Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni kumeibuka kundi kubwa tu la
watu wenye busara na elimu zao lakini wepesi wa kuvutiwa na vitu vya
'kipuuzi' - umbeya, matusi, majungu, na upuuzi mwingine, na hawasiti
kushea na wanaowa-follow. Ni hivi, mtu akitweet tusi, kisha
ukali-retweet, utambue kuwa unalikuza (amplify) tusi hilo. Na kimsingi,
kwa kiasi kikubwa, tuna-RT vitu tunavyoviunga mkono. Uki-RT tusi maana
yake unaliunga mkono. Na ni wazi mwenye kujiheshimu, na kuheshimu 'watu
wa maana' wanaom-follow hawezi ku-RT upuuzi.
Tatizo kubwa sasa ni kwamba waweza kuamua kuwa-follow watu unaodhani
wana busara au akili za kutosha lakini ukaishia kusoma vitu vya ajabu
ajabu kwenye timeline yako kutokana na haya 'mahaba' ya ku-RT vitu vya
kipuuzi.
Binafsi, nadhani chanzo kikubwa cha mitandao ya kijamii kuwa 'sehemu za
kukera, kuogopesha, kunyanyasana, nk' ni ile hali ya baadhi ya wenzetu
kutokuwa na vitu muhimu vya kufanya katika maisha yao. Ni wazi kwamba
ukiwa busy na maisha yako hutokuwa na muda wa kubughudhi wenzako.
Kingine kinachopelekea social media kuwa 'dunia uwanja wa fujo' ni
ugonjwa mkubwa unawasumbua baadhi ya wenzetu: kusaka sifa wasizostahili.
Wanasema,. ashakum si matusi, 'lugha ya mpumbavu ni matusi,' na ndo
maana baadhi ya wenzetu wasio na cha maana cha kuongea katika hadhara
hukimbili matusi, unyanyasaji, maneno macha
Nitamke bayana kuwa siandiki makala hii nikitegemea kuungwa mkono na
wahusika wa unyanyasaji mtandaoni. Na kwa hakika kuna uwezekano mkubwa
wa makala hii kuzua 'kampeni ya chuki' dhidi yangu kutokana na makala
hii. Tatizo kubwa la wenzetu hawa ni kutotaka kuambiwa kuwa 'Hapana,
hili ni kosa. Na kosa ni kosa, haliwezi kuwa sahihi.' Lakini pamoja na
uwezekano wa 'kuwashiwa moto' kutokana na makala hii, wito wangu kwa
kila mwenye busara na akili ni kuliangalia tukio hili la kusikitisha
kama 'wake up call.' Tujifunze, tujisahihishe. Tuache kusherehesha vitu
vya kipuuzi mtandaoni.
Ifike mahala, ukishindwa kumkemea mtu mwenye tabia mbaya mtandaoni basi
chukua option rahisi ya kum-unfollow au ikibidi kum-block. Na ifike
mahala kuwafahamisha watu wanaoendekeza utoto, majungu, umbeya,
unyanyasaji na upuuzi mwingine kuwa kama hawana kitu cha maana cha
kufany katika maisha yao basi isiwe sababu ya kuwasumbua wenzao wenye
majukumu katika maisha yao.
Tukemee maovu badala ya kutarajia yataondoka yenyewe tu. Tuomboleze kifo
cha Betty kwa kusema 'NO' kwa cyberbullies (wanyanyasaji wa mtandaoni).
Tufike sehemu tuache kuwasujudia wahuni wanaodhani matusi ni sehemu ya
wimbo wa taifa. Tuwakwepe waendekeza majungu, wanyanyasaji, wataka sifa
za kipuuzi, na watu wasiofaa katik maisha yetu.
Wakati 'tunatafuta haki kwa marehemu Betty kutokana na unyama
aliofanyiwa,' suala ambalo ni la kisheria, kilicho ndani ya uwezo wetu
ni kukemea unyanyasaji mtandaoni (cyber bullying). Wakati hadi muda huu
hatuwajui waliomfanyia marehemu unyama huo, takriban sote twawajua vema
wanyanyasaji wa mtandaoni. Tuanze na hawa, kwani leo wamefanya kwa kwa
marehemu Betty kesho itakuwa kwako.
Mwisho kabisa, ni muhimu kwetu sote kutambua kuwa tulitoka kwa udongo na
tutarudi kwa udongo. Kifo ni hatma ya kila mmoja wetu.Betty ametutoka
lakini nasi twaelekea huko. Visa, chuki, kunyanyasana, na vitu vingine
visivyopendeza japo ni kama sehemu ya maisha yetu havipaswi kupewa
nafasi katika maisha yetu haya ambayo hakuna mmoja wetu mwenye japo
'lue' ya lini yatafikia kikomo. TUPENDANE na TUHESHIMIANE.
Kwako marehemu Betty, hakuna tunaloweza kusema au kufanya sasa kurejesha
uhai wako. Na hakuna neno sahihi la kuonyesha jinsi gani kifo chako
kimewagusa wengi. Kubwa tunaloweza kufanya ni kukuombea kwa Mwenyezi
Mungu akupatie pumziko la milele na mwanga wa milele akuangazie upumzike
kwa amani. Amina.
Evarist Chahali
No comments:
Post a Comment