Kugombana
ni jambo ambalo halikwepeki katika uhusiano wa kimapenzi. Upo ugomvi
ambao ni wa kawaida na huisha kirahisi lakini upo ugomvi ambao huwa
mkubwa na kama ukitokea na ukashindwa kujua nini cha kufanya kuweka
mambo sawa, husababisha ufa kwenye penzi lenu.Leo
tutazungumzia mambo muhimu ya kufanya inapotokea wewe na mpenzi wako
mmeingia katika ugomvi mkubwa, mmetoleana maneno machafu au hata
kupigana.
1. TAFAKARI CHANZO CHA TATIZO
Kuna usemi kwamba
ukitaka kulitatua vizuri tatizo ni lazima kwanza ujue chanzo cha tatizo
lenyewe. Ukishindwa kugundua chanzo cha tatizo, basi na wewe unakuwa
sehemu ya tatizo.
Utashangaa kwamba wapenzi wengi hugombana na
mambo kuwa makubwa kabisa kwa sababu ya vyanzo vidogo ambavyo
walishindwa kuvigundua mapema na matokeo yake vikazaa matatizo mengine.
Mfano rahisi, chanzo kinaweza kuwa mpenzi wako amekupigia simu lakini
ukashindwa kuipokea kwa muda muafaka. Atakapopiga kwa mara nyingine au
mkikutana, usitegemee atakufurahia kwa sababu atahisi umemdharau kwa
kutopokea simu yake.Endapo ukifanya makosa ya kushindwa kuliona kosa
lako mapema na kushindwa kuomba radhi au kutoa maelezo yanayoeleweka kwa
nini hukupokea simu, matokeo yake utamjibu vibaya, naye atakujibu
vibaya na mwisho mtaishia kupigana au kuachana kabisa mkiwa mmeshatoka
kabisa kwenye kosa la msingi.
Bila shaka msomaji wangu umeona jinsi chanzo kidogo kinavyoweza
kusababisha tatizo kuwa kubwa. Ndoa nyingi au uhusiano unaofika mwisho
huwa umesababishwa na mambo madogo ambayo yalishindwa kutafutiwa suluhu
mapema.
Katika kila ugomvi unaotokea, jambo la kwanza jipe muda wa kutafakari
chanzo kilichosababisha mkagombana. Wakati mwingine wewe ndiyo unaweza
kuwa chanzo cha tatizo lakini kama ukiyajua makosa yako mapema na kukiri
kisha kuomba radhi kwa mwenzio, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya
kurudisha mapenzi kwa haraka.
2. MPE MUDA HASIRA ZIISHE
Kila binadamu ameumbwa
akiwa na hasira na kwa bahati mbaya ni wachache wanaoweza kuzidhibiti
hasira zao. Ni rahisi mtu kutukana, kupiga au kuharibu vitu akiwa na
hasira.Baada ya kugombana, kila mmoja lazima atakuwa na hasira na njia
pekee inayoweza kuepusha matatizo zaidi, ni kujipa muda na kumpa muda
mwenzako ili hasira zipungue.
Kama mpo sebuleni na umetokea ugomvi, ni busara kwenda chumbani au
nje mpaka hasira zako zikiisha. Ni makosa kulazimisha suluhu wakati kila
mmoja akiwa na jazba kwani mtaishia pabaya zaidi.
Ukishaona hasira
zako zimetulia na mwenzako naye ametulia, unaweza kuanzisha mada juu ya
kilichosababisha mkagombana. Tumia lugha ya upole kwani endapo utakuwa
ukifoka au kuzungumza kwa sauti ya juu, matokeo yake mtarudia tena
kugombana.
3. MPE NAFASI YA KUZUNGUMZA
Huwezi kumuelewa mtu
kabla hujampa nafasi ya kuzungumza na kumaliza kile alichokusudia
kukisema. Endapo tatizo limetokea na upo kwenye hatua za kusaka suluhu,
mpe mwenzako nafasi ya kueleza dukuduku lililopo ndani ya moyo wake.
Usimkatishe
wala kumbishia chochote, muache aongee ulichomuudhi mpaka dukuduku lake
liishe kisha na wewe jieleze kwa upole na sauti tulivu.
4. OMBA MSAMAHA
Hakuna silaha nzuri inayoweza
kukusaidia kuushinda ugomvi wowote na kutuliza mambo kabla hayajawa
mabaya kama kuomba msamaha. Neno ‘samahani’ ni dogo lakini lina maana
kubwa kwa yule mtu anayelitoa na anayelipokea.
Hata kama unaona dhahiri kwamba kosa siyo lako, omba msamaha kwanza
kisha baada ya hapo anza kumuelewesha mpenzi wako kwa upole. Lazima
mwisho na yeye atayaona makosa yake na kukuomba msamaha, mtaweza kuepuka
kuukuza ugomvi huo na kurudisha hisia za mapenzi.
5. USIWEKE KINYONGO
Endapo umeamua kuomba
msamaha kwa mpenzi wako, au yeye amekuomba msamaha, samehe kwa dhati
kutoka ndani ya moyo wako na sahau kile kilichotokea. Ni kosa kubwa
kuweka kinyongo rohoni, yaani unamwambia kwamba umemsamehe wakati moyo
wako bado una hasira naye. Ukisamehe kwa dhati, jifunze na kusahau kwani
kusamehe kunaenda sambamba na kusahau.
Wazungu wanasema forgive and forget. Elewa kwamba mpenzi wako ni binadamu ambaye hajakamilika, wala si malaika.
Lazima atakuwa akikosea mara kwa mara, endapo utakuwa ukilimbikiza
vinyongo, unafuga matatizo makubwa kwani siku nyingine akikukosea hata
jambo dogo, utakumbushia na ya jana na juzi na mwisho ugomvi utakuwa
mkubwa sana.
No comments:
Post a Comment