Makala : Gladness Mallya
NIWASHUKURU wote tulioanza nao makala haya ambayo
mwigizaji Wastara Juma amekuwa akifunguka kuhusiana na maisha yake, bila
shaka kwa namna moja au nyingine tutakuwa tumejifunza kitu kupitia
maisha yake.
Leo tunamalizia sehemu ya mwisho ya makala haya, tutaona jinsi gani
alikutana na aliyekuwa mumewe, marehemu Juma Kilowoko ‘Sajuki’. Twende
pamoja:
Mwandishi: Ulikutana lini na Sajuki na wapi?
Wastara: Nilikutana na Sajuki mwaka 2007 kwenye kazi ya filamu ambapo
tulikuwa marafiki sana, mara nyingi tulikuwa tunakaa na kuzungumza
stori za maisha huku kila mmoja akimweleza mambo aliyopitia katika
mapenzi, ile filamu ilipoingia tu sokoni tukaanzisha uhusiano kwani kila
mtu alikuwa na ‘stress’ za mapenzi na kila mmoja alikuwa ameshajua
anachokipenda na anachokichukia mwenzake.
Wastara: Kwa hiyo uhusiano tuliuanza rasmi mwaka 2008 ambapo tulikaa
mpaka 2009 ndipo tukafunga ndoa, kabla ya ndoa wakati tukiwa tunaenda
kulipia ukumbi mimi na Sajuki, tulipata ajali nikavunjia mguu.
Mwandishi: Maisha ya ndoa kwa Sajuki yalikuwaje?
Wastara: Ukweli yalikuwa mazuri kwani alikuwa ni mwanaume ambaye
nilikuwa namhitaji kwani alikuwa na sifa zote, alikuwa ananipenda na
ananijali kwa kila kitu lakini ndiyo hivyo Mungu amemchukua.
Mwandishi: Mpaka sasa kwenye kampuni yenu (WAJEY) mna filamu ngapi?
Wastara: Tuna filamu 16 na za kushirikishwa ni 9 na nimeshirikishwa
chache sababu mara nyingi Sajuki alikuwa anapenda tucheze za kwetu tu.
Mwandishi: Ni kitu gani kizuri ambacho kiliwahi kukutokea na hutakisahau maishani?
Wastara: Siwezi kusahau siku niliyopata Tuzo ya Mwigizaji Bora wa
Kike kutoka Global Publishers kupitia gazeti la Risasi kwani mpaka sasa
hajawahi kutokea mwingine hivyo najiona niko bora mpaka leo.
Mwandishi: Katika maisha yako starehe yako kubwa ni nini?
Wastara: Ukweli starehe yangu kubwa ni mapenzi kwani nikiwa na mpenzi
huwa najisikia starehe na huwa ninayaheshimu sana mapenzi kuliko kitu
chochote kwani yanafanya akili yangu iwe sawa hivyo hata sasa ukiona
siko sawa ni kwamba sijapata mwanaume wa kunistarehesha huwa na sipendi
mapenzi ya wanafunzi.
Mwandishi: Je unampenda mwanaume mwenye sifa gani?
Wastara: Nampenda mwanaume mwenye mapenzi na watoto kwani nina watoto
tayari, atakayenipenda mimi kama Wastara na siyo kwa kuniona kwenye
picha kwani nina ulemavu tayari pia kubwa zaidi nahitaji atakayenipa
muda wake na siyo ambaye anakuwa bize na simu muda wote au kushinda
mitandaoni.
Mwandishi: Je una mchumba na unatarajia kuolewa lini?
Wastara:
Ukweli sina mchumba na hata sijawaza ila mume wangu Sajuki akimaliza
miaka miwili tangu alipofariki dunia ndipo nitaanza kuwa na wazo la kuwa
na mchumba.
Mwandishi: Vipi kuhusu huyu Bond Bin Sinan ambaye anatajwa kuwa
amerithi mikoba ya Sajuki? Wastara: Hakuna yule ni mtu wa karibu yangu
katika masuala ya kazi tu pia ni meneja wangu, hakuna kinachoendelea nje
ya sanaa.
No comments:
Post a Comment