Nianze
kwa kumshukuru Mungu ambaye ameniweka hai mpaka siku hii ya leo,
tunapokutana tena kwenye uwanja wetu huu kujuzana, kujadiliana,
kuelimishana na kuzungumzia ishu mbalimbali zinazohusu uhusiano wa
kimapenzi.
Leo
nataka kuzungumza na wewe mama, dada, shangazi au mwanamke ambaye upo
kwenye uhusiano wa kudumu, nikimaanisha umeolewa. Je, umewahi kugundua,
kuhisi au kuambiwa kwamba mumeo mliyeishi pamoja kwa kipindi kirefu,
amezaa mtoto na mwanamke wa nje?
Bila shaka kila mmoja atakuwa na majibu yake lakini katika mada hii
nataka kuzungumza zaidi na wahusika, wanawake ambao wamewahi kutokewa na
tatizo hili. Ni ukweli usiofichika kwamba wanaume wengi siku hizi
wamekuwa na mchezo wa kuzaa nje ya ndoa.
Yaani amekuoa na mnaishi pamoja kama mume na mke, mmejaliwa kupata
mtoto au watoto lakini kumbe nyuma ya pazia, yupo mwanamke mwenzako
ambaye naye amezalishwa na mumeo. Je, unapaswa kufanya nini katika
mazingira kama haya?
Mada ni nzito na ndiyo maana napenda zaidi kusikia kutoka kwa
waliotokewa na tatizo hili kwani naamini kupitia wao, wengine
watajifunza na hata watakapokuja kutokewa na hali kama hii, watajua
namna ya kupambana nalo.
Je, ukigundua mumeo ana mtoto nje ya ndoa, utadai talaka, utamtafuta
mwizi wako mpaka umpate na kumshikisha adabu, utamsaka mtoto ili umdhuru
au utafanya nini? Hebu sikiliza ushuhuda wa mwanamke huyu ambaye
nimewahi kukutana naye, akanisimulia mkasa wake ambao leo ndiyo
ulionisukuma kuja na mada hii.
“Mimi ni mwanamke ambaye nimeolewa miaka minne iliyopita na
kufanikiwa kupata watoto wawili. Wa kwanza ana miaka mitatu na huyu
mwingine bado hajafikisha hata mwaka mmoja. Mume wangu ni mfanyakazi wa
kampuni moja kubwa jijini Dar es Salaam.
Kwa kipindi chote tangu tuoane, tumekuwa tukiishi kwa amani na upendo
wa hali ya juu mpaka miezi michache iliyopita ambapo nimegundua jambo
baya mno katika ndoa yangu.“Nimegundua kwamba mume wangu ana mtoto
mwingine ambaye ana umri wa miaka miwili.
Huyo
mwanamke aliyezaa naye, mwanzo walikuwa wakifanya kazi pamoja ingawa
sasa nasikia hayupo tena kazini kwa mume wangu ila nimesikia tetesi
kwamba mume wangu ndiye aliyempangia chumba na anamhudumia kila kitu na
siku nyingine huwa anaenda nyumbani kwake.
Nipo njia pandaa najihisi nakaribia kupatwa na ugonjwa wa moyo, ndoa
yangu naiona chungu, namchukia sana mume wangu japokuwa ameniomba
msamaha, sidhani kama nitamsamehe, naomba ushauri, nifanyeje?”
Hayo ndiyo maelezo aliyonipa mwanamke huyo ambaye kiumri bado ni
mbichi na ndoa yake ndiyo hiyo ina miaka minne. Mpendwa msomaji wangu,
bila shaka umeyaelewa vizuri maelezo ya dada huyu na tayari unayo majibu
ya kumpa. Je, utamshauri nini?
KOSA LA MSINGI
Kosa la msingi ambalo mume wa dada huyu
alilifanya ni usaliti. Yaani licha ya mwenzake kumpenda kwa moyo wote,
aliamua kuchepuka na kwenda kwa mwanamke mwingine na kumpa ujauzito,
kosa juu ya kosa.
Kosa la usaliti pekee ni baya na kama tulivyowahi kuzungumza kipindi
cha nyuma, humchukua muda mrefu sana mtendewa wa usaliti kurudi kwenye
hali yake ya kawaida na kurejesha mapenzi kwa aliyemtenda. Wengine
hujikuta wakishindwa kabisa kusamehe na kusahau yaliyotokea.
Inapotokea usaliti umesababisha mtoto wa nje, uzito wa kosa huwa
mkubwa zaidi na hata namna ya kulishughulikia, ni lazima wanandoa wote
wawe makini sana kwani vinginevyo, huo unaweza kuwa mwisho wa ndoa au
mapenzi kati ya wawili hao.
No comments:
Post a Comment