Wednesday, 22 October 2014

MBEYA::KANDORO AYASHUKIA MAKAMPUNI YANAYONYANYASA WAKULIMA.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro,  alipokuwa akizindua umoja wa Wakulima wa Mpunga (MTAYArF) unaoziunganisha Kampuni za Mtenda rice , Tanseed na Yara katika sherehe zilizoenda sambamba na mafunzo kwa Wakulima wa Mpunga Mkoa wa Mbeya zilizofanyika katika ukumbi wa Mtenda Sun Set uliopo Soweto jijini hapa.
Mkurugenzi wa Mtenda Kyela Rice Company ltd, George Mtenda, alisema lengo la kuungana ni kuwapunguzia gharama wakulima za upatikanaji wa pembejeo bila kupitia kwa madalali jambo ambalo litamsaidia Mkulima kutengeneza faida moja kwa moja.
 Mwenyekiti wa Bodi ya MTAYArF, Stella Mutagwaba, akisoma risala mbele ya mgeni rasmi
Wakulima wa Mpunga Mkoa wa Mbeya na wadau wa kilimo wakimsikiliza mkuu wa mkoa Mbeya
Picha ya pamoja



MAKAMPUNI  yanayofanya shughuli sambamba na wakulima nchini  yametakiwa kuwa na mikataba ambayo itawanufaisha moja kwa moja wazalishaji ili waondokane na kilimo kisichokuwa na tija kwao.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro,alitoa wito huo  alipokuwa akizindua umoja wa Wakulima wa Mpunga (MTAYArF) unaoziunganisha Kampuni za Mtenda rice , Tanseed na Yara katika sherehe zilizoenda sambamba na mafunzo kwa Wakulima wa Mpunga Mkoa wa Mbeya zilizofanyika katika ukumbi wa Mtenda Sun Set uliopo Soweto jijini hapa.
Kandoro alisema mara nyingi makampuni yanaingia ubia wa kushirikiana na Wakulima kwa lengo la kutengeneza faida kwa kuwanyonya na kutengeneza mikataba ambayo ni kandamizi kwa Mkulima na kuishia kuwa mtumwa dhidi ya kampuni husika kupitia mikopo ya pembejeo.
Alisema Makampuni huingia makubaliano na wakulima kwa lengo la kuwakopesha pembejeo lakini huwalazimisha kununua mazao wao wenyewe tena kwa kujipangia bei ambayo haimletei mafanikio Mkulima hivyo kushindwa kuendelea licha ya kuzalisha mazao mengi.
Alisema tabia hiyo haipaswi kuvumiliwa jambo ambalo Serikali inasisitiza wakulima kujiunga kwenye vikundi ili iwe rahisi kukopeshwa pembejeo kupitia vikundi vyao ambapo alitoa rai kwa umoja wa Mtayarf kufanya kazi na vikundi na sio mkulima mmoja mmoja ili kuepuka hujuma.
Aidha mbali na kutoa wito huo pia aliwapongeza wamiliki wa Makampuni hayo kwa kuanzisha umoja ambapo alisema kama utafanya  vema utasaidia kutoa mafunzo kwa wakulima jambo litakalochangia kuongeza uwezo wa uzalishaji na kuwatafutia masoko ya mazao yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mtenda Kyela Rice Company ltd, George Mtenda, alisema lengo la kuungana ni kuwapunguzia gharama wakulima za upatikanaji wa pembejeo bila kupitia kwa madalali jambo ambalo litamsaidia Mkulima kutengeneza faida moja kwa moja.
Awali katika risala iliyosomwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Mwenyekiti wa Bodi ya MTAYArF, Stella Mutagwaba, alisema muungano huo ni wa kampuni tatu zinazotoa huduma katika mnyororo wa thamani wa zao la mpunga na wakulima wa Mpunga wilaya za Kyela, Mbarali na Momba.
Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Kampuni ya ununuzi wa Mpunga, usindikaji wa Mpunga na uuzaji wa mchele(Mtenda Kyela Rice supply companyltd),Kampuni ya mbegu(Tanseed international ltd) na Kampuni ya Mbolea ya Yara Tanzania ltd.
Mwisho.


Na Mbeya yetu

No comments:

Post a Comment