Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu
Aliyekuwa
mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu,
ametoboa siri kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Joseph Warioba alikuwa
na msimamo wa serikali mbili, kabla ya tume kuja na rasimu yenye muundo
wa muungano wa serikali tatu uliotokana na maoni ya wananchi walio
wengi.
Baregu alitoboa siri
hiyo wakati akizungumza na NIPASHE katika mahojiano maalum yaliyofanyika
nyumbani kwake mwanzoni mwa wiki hii. Alikuwa akijibu moja ya maswali
aliyoulizwa kuhusiana na namna wao (tume) walivyoondosha tofauti za
kimtazamo miongoni mwa wajumbe na kuandaa rasimu iliyokubaliwa na
wajumbe wote; tofauti na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ambayo
walitofautiana sana kuhusiana na suala la muundo wa muungano na
mwishowe, wajumbe wengi wa upinzani wakasusia vikao kupitia mwavuli wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kuwaachia wenzao wanaoundwa na
wafuasi wengi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuendelea na kazi hiyo.
Wajumbe wanaounda
Ukawa ambao wengi ni kutoka vyama vikuu vya upinzani nchini vya
NCCR-Mageuzi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha
Wananchi (CUF) walisusia vikao vya Bunge la Katiba kutokana na madai yao
kuwa rasimu iliyoandaliwa na tume iliyoongozwa na Warioba kwa
kuzingatia maoni ya wananchi ilibadilishwa kwa maslahi ya CCM. Ukawa
walikuwa wakitetea rasimu ya Warioba iliyopendekeza muundo wa muungano
wa serikali tatu huku wajumbe wengi wa CCM wakisisitiza kuwa na muundo
wa muungano wa serikali mbili lakini ulioboreshwa.
Akieleza zaidi, Baregu
alisema kuwa kwa ujumla, tume ilijigawa kwenye kamati ndogo tatu wakati
wa kuanza kujadili mapendekezo, ambazo ni kamati ya mihimili ya utawala
(bunge, serikali na mahakama), kamati ya iliyokuwa ikishughulikia
misingi na maadili ya taifa na kamati ya tatu ndiyo iliyokuwa
ikishughulikia masuala ya muungano.
“Labda niwaeleze tu,
hiyo kamati ya muungano tuliipa jina kama kundi la kifo... na ninalitaja
kundi hili kwa masikitiko kwa sababu mmoja wetu, Dk. Mvungi alifariki
kweli,” alisema.
Prof. Baregu alisema
kundi la kifo lilikuwa la watu wenye misimamo kuanzia wa serikali moja,
mbili, tatu na wengine waliokuwa na mawazo ya kuwa na muungano wa
mkataba.
“Akina nanihii hawa...
akina Warioba, akina Butiku, Jaji August... walianza na msimamo wa
serikali mbili. Mimi siku nyingi ni mtu wa serikali moja. Wakawapo watu
wa serikali tatu, including (akiwamo) Dk. Mvungi. Na kundi la nne la
watu wenye msimamo wa serikali ya mkataba,” alisema.
Alisema pamoja na
minyukano iliyojitokeza kutokana na misimamo hiyo binafsi ya wajumbe,
bado waliweza kusimama imara na kuzishinda nafsi zao kutokana na mawazo
ya wananchi waliyoyapata wakati wakikusanya maoni katika maeneo
mbalimbali nchini, chini ya uongozi wa mwenyekiti wao (Warioba).
Alisema kuwa awali,
mwenyekiti wao (Warioba) alitoa nafasi kwa kila mjumbe kwenye suala la
muungano kuzungumza na kutoa mchango wake.
“Ninakumbuka kwenye
issue hii ya muungano, kila mjumbe ilibidi azungumze. Na mwenyekiti
ali-insist kwamba kila mmoja wetu ni lazima achangie, na tukalizungumza
kwa karibu wiki nzima,” alisema.
Prof. Baregu alisema
pamoja na kila mjumbe kuzungumza, pia waliangalia maoni waliyokusanya
kutoka kwa wananchi na mwisho wa siku wakaja na maamuzi ya pamoja,
ambayo yaliwafanya kuchukua msimamo wa pamoja pia.
Alisema hawakumuacha
mjumbe yeyote nyuma akiwa bado hajaridhika kwa hoja na maoni
waliyokusanya na kwamba, pale ilipotokea hivyo, walianza naye kwenye
kikao kilichofuata hadi kuhakikisha kwamba mhusiaka ameridhika.
“Na ndiyo maana sasa
hivi ukizungumza na wajumbe wote, sijasikia hata mmoja ambaye
amebadilisha mawazo, ama... au amesema kwamba alirubuniwa kwenye tume au
labda kwamba Jaji Warioba alifanya maamuzi ya ubabe,” alisema.
Alisema kutokana na
namna walivyoendesha mambo yao kwa uwazi na kufikia maamuzi ambayo wote
waliyaafiki kikamilifu kuwa yamezingatia kwa usahihi matakwa ya
wananchi, ndiyo maana bado wana mshikamano mzuri hadi sasa na wameamua
kwenda kuitetea rasimu ya tume kwa wananchi.
Amesisitiza kuwa
wajumbe wa tume hiyo wamejipanga kuhakikisha wanawaelimisha wananchi
kuhusu mapendekezo yaliyokuwa kwenye rasimu hiyo.
Alisema walipokuwa kwenye Tume walifanyakazi kwa bidii, weledi, nidhamu na kujenga maridhiano ndani ya jamii na ndani ya tume.
"Tuliwasikiliza
wananchi wanataka nini na kuzingatia maoni ya Watanzania, na lengo la
tume lilikuwa ni kupata katiba yenye maoni ya wananchi,” alisema.
KATIBA ILIYOPENDEKEZWAAlisema
sasa hivi, kwenye Katiba iliyopendekezwa, kuna mambo mengi ya msingi
yamenyofolewa; kama mambo ya maadili, uwajibikaji, kumwajibisha mbunge,
ukomo wa ubunge, madaraka ya rais na mawaziri kutokuwa wabunge; mambo
ambayo yalipendekezwa na wananchi wengi.
Prof. Baregu alisema
njia pekee ya kunusuru mchakato mzima wa katiba ni kukubali kwamba
tumekwama na kukubali kusahihisha makosa badala ya kuburuza mchakato huo
bila maridhiano.
Katiba iliyopendekezwa
ilikabidhiwa juzi mjini Dodoma kwa marais, Jakaya Kikwete wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Dk. Ali Mohamed Shein wa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar.
“Sisi ndani ya Tume tulijenga kwanza maridhiano ndiyo maana tuliweza kutoa rasimu ambayo sote tulikubaliana,” alisema
Prof. Baregu alisema:
"Kwa hali hii, ilipaswa tuwe na ujasiri wa kupumua kwanza, tukaulizana
na tukakubali kwamba tumekwama kwa malengo tuliyokuwa tumejiwekea...
sasa hivi ni kama mtu umepotea njia lakini unasema twende tu."
Aliongeza kuwa:
"Tulikuwa na lengo, tulikuwa na ramani kwa hiyo kama tungekuwa na
ujasiri kama taifa tukasema ngoja tujiulize hapa tufanye nini ili tuweze
kutoka hapa, mengi tungeweza kubadilisha." Alisema mchakato umekwama
baada ya kutawaliwa na wanasiasa ambao hawawezi kupitisha mapendekezo
ambayo yanapingana na maslahi yao.
"Ni vyema kama
tungekubali kusema hapa tumekosea, tuunde upya Bunge la Katiba, na
kukubali kwamba tumekosea sana... na siyo serikali tu, lakini sote kama
taifa."
Alisema. "Nimekuwa
nafikiri hivi... ni kama mama mwenye mimba anayepata abortion (mimba
kuharibika). Anajisikiaje?” alisema Baregu.
Alisema kwa hali
ilivyopelekwa, anahisi kuwa na hali kama hiyo ya mama aliyeharibikiwa na
mimba yake, kwamba amekuwa kwenye timu iliyofuatilia watu karibu mwaka
mmoja na nusu kutunga katiba, lakini inaishia kusakamwa.
Alisema tume imefanya kazi kwa uadilifu, weledi
No comments:
Post a Comment