Thursday 4 September 2014

IJUE HISTORIA NA MGUNDUZI WA 'THE MAGIC SPRAY' INAYOTUMIKA VIWANJA VYA SOKA DUNIANI

September 4, 2014
Huyu ndiye mtengenezaji wa aina mpya ya kinyunyizio ‘9-15’, Muargentina Pablo Silva.
Kinyunyizio hicho kikitumika katika baadhi ya mechi.
Aina mpya ya kinyunyizio ‘9-15’.
KWA mara ya kwanza kuona marefa wa mpira wa miguu wanabeba kinyunyizio ‘spray’ kwa wengi wetu ilikuwa ni kipindi cha Kombe la Dunia lililofanyika miezi mitatu iliyopita nchini Brazil.
Historia inaonesha jinsi gani kinyunyizio kilivyogunduliwa enzi za miaka ya 1980 na baadhi ya wachezaji kama Sir Bobby Charlton na refa Neil Midgely kuuomba uongozi wa FA kuiruhusu kutumika katika Ligi Kuu ya Uingereza bila ya mafanikio. Uzinduzi huu ulishawahi kufika mpaka ofisi za Adidas kwa muendelezo na bado wazo hili lilipigwa chini pia.
Mwaka 2000, Mbrazili mbunifu, Heine Allemagne alitengeneza /kuboresha kifaa kama hicho na kukiita “Spuni” ambayo kwa mara ya kwanza ilitumika rasmi katika ligi kuu ya nchini humo (Brazil) mwaka huo huo.
Na baada ya hapo marefa waliungana mkono katika utumiaji wa kinyunyuzio hicho na hivyo kuanza kukubalika katika mpira wa miguu huko America ya Kaskazini. Kuanzia kipindi hicho kinyunyizio hicho kilionekana kutumika katika mapambano ya kimataifa (International Football Competitions) mbalimbali.
Juni 2014 aina mpya ya kinyunyizo iliyotengenezwa na Muargentina Pablo Silva na kuitwa ‘9-15’ ikimaanisha umbali wa kupiga mpira wa adhabu ndogo na ukuta wa kuzuia, kilianza kuonekana kimataifa katika matangazo ya Kombe la Dunia 2014 yaliyotoka kufanyika miezi mitatu iliyopita licha ya kuwa na matangazo ya bidhaa hiyo tokea mwaka 2008.
Copa America ya mwaka 2011 ndiyo ulikuwa mwanzo wa kutumika kwa bidhaa hiyo kwa ngazi za kimataifa na hatimaye kuanza kutumika rasmi na ligi nyingine za nje kama MLS ya Marekani Kusini, Kombe la Dunia 2013 chini ya miaka 20, Ligi ya Uturuki, Ligi ya Mabingwa Ulaya chini ya miaka 17 na Kombe la Dunia 2014.
Ama kweli subira ya vuta heri, baada ya miaka 14 sasa kinyunyizio hicho kinatumika katika ligi kubwa zote ikiwemo Bundesliga ya Ujerumani, Seria A ya Italia, Ligue 1 Ufaransa, La Liga ya Hispania, Premier League Uingereza na A-League ya Australia.
Bwana Pablo Silva unakaribia kuwa tajiri wa kufa mtu lakini hatuna budi kukushukuru kwa uvumbuzi wa karne mpya uliotuletea. Kila la kheri.
(Na ‘Mpenda Michezo’ / GPL)

No comments:

Post a Comment