Na Shakoor Jongo SIKU
chache baada ya kutolewa kwa taarifa ya kukamatwa kwa promota
aliyempeleka msanii Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ nchini Ujerumani kwa
ajili ya kufanya shoo aliyejulikana kwa jina la Awin Williams
Akpomiemie, mwenye asili ya Kinigeria, nyuma ya sakata hili siri saba
zimefichuka, Risasi Jumamosi lina ripoti kamili.
Mashabiki wenye gadhabu wakilizingira gari la Mbongo Fleva, 'Diamond Platinum' nchini Ujerumani.
SIRI YA KWANZA; KIBALI Uchunguzi uliofanywa na
mwanahabari wetu ulibaini kwamba katika sakata hilo lililojiri wiki
mbili zilizopita, promota huyo aliwadanganya wamiliki wa Ukumbi wa
Sindelfingen uliopo Mji wa Stuttgart, Ujerumani kuwa kutakuwa na mkutano
wa Waafrika waishio nchini humo na baada ya hapo kutakuwa na pati ya
kawaida.
Ilisemekana kwamba wamiliki hao walitoa kibali kwa ajili ya mkutano
hivyo walishtushwa kuona ukumbi umejaa na watu wanamsubiri Diamond
kinyume na makubaliano.Kikizungumza kwa njia ya simu kutoka nchini humo,
chanzo chetu kilidai kwamba ujanja alioutumia Awin kuwadanganya
wamiliki wa ukumbi huo ndiyo chanzo cha fujo hiyo kwani alishindwa
kuanza shoo mapema kwa kuwa wamiliki wa ukumbi hawakuwa tayari kwa jambo
hilo.
Magari ya wagonjwa yakiwa tayari kuhudumia majeruhi eneo la tukio.
“Unajua siyo kila mtu anataka kuishi kwa shaka huku Ujerumani. Kila
mtu anajua maisha ya Waafrika jinsi wanavyoishi, sasa uongo ungebainika
mapema sidhani kama tungeishi kwa raha,” kilidai chanzo hicho.
SIRI YA PILI; UTEKAJI Habari kutoka nchini humo
zilidai kwamba siri ya pili ni kwamba Diamond alikuwa atekwe kwani
kulikuwa na waandaaji watatu wa mpango huo hivyo wawili walitaka kumteka
msanii huyo ili akafanye shoo sehemu nyingine.
“Mbali na Awin kulikuwa na jamaa wengine wawili ambao waliingilia
mchakato mwishoni wakitaka waandae shoo hiyo lakini mwishoni
walitofautiana ‘so’ walitaka waharibu ndiyo maana Diamond akachelewa
ukumbini na vurugu zikatokea,” kilitonya chanzo chetu.
Mkali 'Diamond' akisepa kutoka eneo la tukio.
SIRI YA TATU; BIMA Kikiendelea kutiririka,
chanzo hicho kilidai kwamba ukiachana na uongo wa promota Awin
iligundulika kwamba hakukuwa na bima ya kulinda usalama wa watu hasa
endapo lingetokea tatizo kama lililotokea ambapo wengi walijeruhiwa.
“Huku Ujerumani huwezi kufanya onesho lolote bila bima ya kulinda
usalama kwenye shoo yako, sasa jamaa hakuwa nayo, kosa ambalo ni kubwa
sana kwa sheria za Ujerumani,” alisema mtoa habari wetu.
SIRI YA NNE; UKUMBI WA MIKUTANO Kingine
kilichogundulika ni kwamba hata ukumbi wenyewe ulikuwa wa mikutano na
maonesho ya bidhaa na si wa kufanyia shoo za muziki kama alivyotaka
kufanya yeye.
“Ukumbi wa Sindelfingen, Stuttgart ni wa mikutano na maonyesho ya
bidhaa, haujawahi kutumika kwa shoo kama ile ndiyo maana hata sisi
tulishangaa iweje utumike kwa ajili ya shoo ya Diamond?” kilihoji chanzo
chetu.
Moja ya shoo aliyofanikiwa kufanya('Diamond') huko majuu.
SIRI YA TANO; HASARA MIL. 600 Chanzo hicho
kilieleza kwamba baada ya uchunguzi wa polisi, ilibainika kwamba hasara
iliyosababishwa na vurugu hizo inafikia euro 300,000 (zaidi ya Sh.
milioni 600 za Kibongo).
“Hicho ndicho kiasi ambacho Awin anatakiwa
kukilipa kwa wamiliki wa ukumbi kwani alisababisha loss (hasara) kubwa
sana,” kilidai chanzo hicho.
SIRI YA SITA; KESI Licha ya promota huyo
kufikishwa polisi kwenye Mji wa Stuttgart, suala lake lipo chini ya
ofisi ya mji huyo ili sheria ichukue mkondo wake huku polisi
wakisisitiza kwamba Diamond akitia mguu tu watamdaka.
“Hadi
ninavyoongea na wewe polisi bado wanamuhoji Awin kutokana na tetesi
kwamba anajihusisha na biashara tata lakini kuhusu fujo zile kesi yake
iko chini ya ofisi ya Mji wa Stuttgart, inavyooneka hali iko vibaya sana
kwa upande wake na Diamond kwani polisi wanakomaa kuwa akitimba tena
watamkamata,” kilisema chanzo hicho.
'Diamond' akiwa na Meneja wake, Babu Tale.
SIRI YA SABA; KUTAFUTA ‘KIKI’ Uchunguzi mwingine
wa gazeti hili ulibaini kwamba sakata la vurugu za Diamond nchini
Ujerumani lilipangwa kwa makusudi ili kutafuta ‘kiki’ (umaarufu) na
kuvuta hisia kupitia vyombo vya habari vya kimataifa ili kumpaisha
zaidi.
“Fuatilia majibu ya meneja wake, Babu Tale. Alisema kuwa vurugu
zilikuwa mbaya lakini ni fagio kwa Diamond kimataifa. Kama siyo kutafuta
kiki ni nini?” kilihoji chanzo makini Bongo na kuongeza:
“Nasikia anarudi Ujerumani kufanya shoo kubwa ya bure (Septemba 20). Wewe huoni hapo kulikuwa na mchezo?”
DIAMOND ANASEMAJE? Alipoulizwa Diamond kuhusiana
na utayari wa yeye kurudi Ujerumani na yote yaliyotokea, hakutaka
kufungukia zaidi ishu hiyo na kudai amejiaandaa vilivyo kufanya shoo ya
bure Septemba 20 kama waandaaji walivyomtaka.
TUMEFIKAJE HAPA Agosti 30, mwaka huu zilitokea
fujo kwenye Ukumbi wa Sindelfingen uliopo Mji wa Stuttgart, Ujerumani
zilizosababishwa na Diamond ambaye alichelewa kupanda stejini hadi saa
10:00 alfajiri ambapo watu walivunja viti, vyombo vya muziki na vitu
mbalimbali baada ya mashabiki kushikwa na hasira kwa kukosa burudani ya
shoo Diamond.