MAISHA
ya kimapenzi, hasa katika nchi masikini kama Tanzania, yamebadili
uelekeo na kuonekana kama ni kitu kinachotanguliza masilahi badala ya
upendo kama ilivyokuwa enzi za mababu zetu.
Enjo, kama alivyojitambulisha kwangu hivi karibuni, anasimulia kisa cha kusisimua.
“Nilikutana
naye kwenye daladala, baada ya kunisalimia tukapiga stori hadi
alipokaribia kushuka katika kituo chake, akaniomba namba ya simu. Kwa
kuwa tulikuwa tumeshazoeana kidogo sikuona taabu, nikampa.
“Aliposhuka tukaendelea kuwasiliana kwa kutumiana sms, kwanza ilikuwa
ni maneno ya kawaida tu, lakini baadaye akabadili na kuanza
kunitongoza. Sikukataa wala kukubali, kwa sababu mtu mwenyewe nilikuwa
simjui.
“Kwa muda kama wa siku mbili hivi tuliendelea kuwasiliana na hatimaye
nikaona acha tu nimkubali. Basi alifurahi sana. Akataka siku tuonane
nikamwambia sawa, tukapanga siku. Kama mara mbili hivi nilimuomba vocha
na alishanirushia ya shilingi elfu tanotano.
“Siku ya ahadi nikamwambia anitumie nauli, akatuma shilingi elfu
kumi, nikaenda sehemu tukakutana. Tukapiga stori sana, tukanywa, tukala,
lakini akanishangaza eti siku hiyohiyo anataka tukafanye mapenzi. Yaani
mtu tumekutana tu leo, hapana, nikamwambia siku nyingine, basi
akalalamika sana na tulipoachana, hakunitafuta tena.”
Simulizi yake iliishia hapo, akaingia Innocent, kijana wa kisasa:
“Nilimuona facebook, nikamuomba urafiki akakubali, tukawa tunachat,
kwanza ilikuwa kawaida lakini baadaye nikamchomekea, akakubali. Basi
tukapeana namba za simu na mawasiliano yakaendelea.
“Siku ya pili tu
akaniomba vocha, nikamwambia aache haraka, mambo mazuri hayataki
haraka. Akasema eti alihitaji kuwasiliana na mama yake aliye mkoani,
nikamwambia atafute maarifa mengine, mimi nafikiria namna ya kumfanyia
mambo makubwa zaidi, hayo madogomadogo kama vocha yatatue mwenyewe.
“Akaniambia eti kama nashindwa vitu vidogo kama vocha, hivyo vikubwa
nitaviweza wapi, nikamwambia subiri utaona. Basi spidi ya mawasiliano
ikapungua, nikimpigia na kumwuliza kwa nini hatumi sms kama zamani,
akaniambia simu yake haina salio.
“Basi
na mimi nikanyamaza, baada ya siku mbili tatu nikampigia na kumwomba
tuonane, akasema kama nitamtumia nauli atakuja, nikamwambia dada mbona
unakompleini vitu vidogovidogo, kama vipi kopa kwa mtu uje
nitakurudishia, akakataa, nikamwambia kama hana nauli basi apotezee.
Nikaachana naye.”
Hizi ni simulizi mbili zenye ujumbe tofauti, lakini zinazowahusu
vijana katika mahitaji yao ya kimapenzi. Wasichana wote wawili
wanaonekana kufanana mahitaji, tofauti na wavulana.
Mvulana wa kwanza alijitahidi kutimiza mahitaji ya mwenza wake
akiamini siku ikifika naye atapewa anachostahili. Lakini yule wa pili
hakuweza kutoa mahitaji ya mwenza wake kwa wakati.
Maisha ya kisasa
yameifanya dunia ya kimapenzi kubadilika sana. Wapo baadhi ya wasichana
wanaoamini mwanaume anayewapenda, lazima ataonyesha kuwajali kwa kuwapa
fedha na mahitaji yao mengine hata kabla hawajakutana kimapenzi.
“Mwanaume gani anashindwa kukutumia hata vocha, mtu anashindwa
kukutimizia mahitaji yako sasa hivi ndiyo ataweza baadaye?” Hili ni
swali unaloweza kukutana nalo kutoka kwa wasichana wengi, wanapozungumza
kuhusu mwanaume wanayemhitaji.
Lakini pia baadhi ya wanaume wamekuwa wagumu kutimiza mara moja
mahitaji ya wasichana. “Yaani hata hajanielewa vizuri, ashaanza kuleta
matatizo yake, kwani kabla hajakutana na mimi vocha alikuwa anapata
wapi. Nimtumie nauli? Kwani si anakuja kwa mpenzi wake anashindwa
kujilipia elfu moja?”
Haya pia ni maswali unayoweza kukutana nayo kutoka kwa baadhi ya
wavulana wanapozungumza juu ya tabia ya wasichana wanaotanguliza
mizinga.
Kuna jambo tunalopaswa kuliangalia vizuri na ikibidi
kujifunza, kitu gani kinatakiwa kutangulia wakati wa uhusiano katika
hatua zake za mwanzo?
Mifano hiyo miwili hapo juu inaweza kuwa mwongozo mzuri kukupeleka
kwenye aina ya uhusiano uupendao. Lakini kwa wasichana, ni vyema sana
kuepuka kutanguliza mahitaji yako yanayohusu fedha, kwani wakati
mwingine wanaweza kujikosesha bahati ya kumpata mtu mwenye malengo ya
maisha kwa vile atamuona ni mtu mwenye kujali pesa badala ya upendo.
No comments:
Post a Comment